Watu 112 wameripotiwa kutoweka huku sakata la MacKenzie likiendelea

Miili 18 zaidi ilifukuliwa Jumapili ikifikisha idadi ya ya miili iliyofukuliwa hadi 39.

Muhtasari

• Watu 112 wamedaiwa kupotea huku shughuli ya ufukuzi wa miili  ya watu wanaodaiwa kufa kutokana na imani potovu ya mhubiri wa Kilifi  Paul Mackenzie ikiendelea.

waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha mauaji na wataalam wa uchunguzi waanza kuopoa miili ya watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kasisi wa Malindi Paul Mackenzie katika eneo bunge la Shakahola Magarini kaunti ya Kilifi.
Image: ALPHONSE GARI

Watu 112 wanaohusishwa na mhubiri mpotovu Mackenzie wameripotiwa kupotea na shirika la Msalaba Mwekundu.

Haya yanajiri huku  uchunguzi dhidi ya mhubiri Mackenzi anayedaiwa kuwapotosha watu kwa madai ya dini ukiendelea. Watu 112 wamedaiwa kupotea huku shughuli ya ufukuzi wa miili  ya watu wanaodaiwa kufa kutokana na imani potovu ya mhubiri wa Kilifi  Paul Mackenzie ikiendelea.

"Tumetengeneza madawati ya ufuatailiaji na ushauri katika hospitali ya kaunti ndogo ya Malindi kwa mwitikio wa Shakahola. Kufikia sasa ,watu 112 wameripotiwa kutoweka kutoka kwenye dawati la ufuatiliaji," Red Cross ilisema kupitia ukurasa wao wa Twitter.

Maafisa  waliokuwa wakifanya uchunguzi na ufukuzi, siku ya Jumapili tarehe 23 Aprili walichimbua miili 18 zaidi ikifikisha nambari ya ya miili iliyofukuliwa hadi 39.

Mhubiri Paul Mackenzie ndiye mshukiwa mkuu katika vifo hivyo vya wingi .Mackenzie ameripotiwa kuwapotosha wafuasi wake  kuwafanya wengine kutoka shuleni na  baadhi kuwacha kazi zao ili kumfuata.

Familia za waliopotea zimetoa wito kwa serikali kutilia mkazo usakaji wa wale wanaojificha katika msitu wa Shalakola huku maafisa wa uchunguzi wakiendelea kupata makaburi zaidi.

Mhubiri huyo anadaiwa kuwarai wafuasi wake kufunga hadi kufa wakitumai kuwa jambo hilo lingefanya wakutane na Yesu kama alivyowaambia mhubiri wao.

Inasemekana kuwa mamia ya wafuasi wa mhubiri Mackenzie kutoka sehemu tofauti tofauti nchini waliwacha manyumba yao na hata wengine kuuza mali yao ili kujiunga na kufunga huko iliyoleta vifo.