Passaris ampongeza Sakaja kwa kuchukua hatua zinazofaa kuboresha hospitali

Mbunge Passaris aliwasifu wateule hao watatu akitaja kuwa wana uzoefu na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Muhtasari
  • Afisa mkuu mtendaji wa AMREF health Africa Githinji Gitahi pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya Mbagathi.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Mwakilishi wa kike Nairobi, Esther Passaris.
Image: Facebook

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja hii leo ameteua wadhifa watatu wakuu katika bodi kadhaa za kaunti.

Aliyekuwa katibu mkuu wa utawala wa afya Mercy Mwangangi aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya Pumwani huku mwanapatholojia wa serikali Dkt. Johansen Oduor akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya wafu Nairobi.

Afisa mkuu mtendaji wa AMREF health Africa Githinji Gitahi pia aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya Mbagathi.

Mwakilishi wa wanawake wa Nairobi Esther Passaris amempongeza gavana Sakaja kwa kuwateua watatu hao kusimamia hospitali za kaunti ya Nairobi.

Mbunge Passaris aliwasifu wateule hao watatu akitaja kuwa wana uzoefu na uwezo wa kufanya kazi hiyo.

Passaris alimshukuru chifu wa kaunti ya Nairobi kwa kuchukua hatua zinazofaa katika kuboresha usimamizi wa hospitali za jiji kwa kuwateua viongozi wenye uzoefu na uwezo.

"Inafurahisha kuona gavana Johnson Sakaja akichukua hatua za kuboresha usimamizi wa hospitali za jiji kwa kuwateua viongozi wenye uzoefu na uwezo kama vile Mercy Mwangangi, Dkt. Johansen Oduor. Ninawatakia kila la heri katika majukumu yao mapya" alitweet Esther Passaris.

Katika notisi ya gazeti la serikali iliyochapishwa mnamo Aprili 28, 2023, Gavana aliteua watu wengine watano kwenye bodi kuhudumu pamoja na CAS wa zamani.

Kulingana na notisi hiyo, Mwangangi atahudumu katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitatu.

“Kikosi kazi kitatayarisha na kuwasilisha ripoti yake kwa Gavana wa Serikali ya Kaunti ya Jiji la Nairobi pamoja na mapendekezo yake ndani ya siku Arobaini na Tano (45) kuanzia tarehe ya uteuzi wake.

"Ofisi ya Gavana itaunda sekretarieti ya Kikosi Kazi," ilisomeka notisi kutoka kwa Sakaja wakati huo.