Reuben Kigame aitaka Azimio isitishe vitisho vya kugawanya Nchi

Alisema haikuwa busara kwa Rais kuwalazimisha Wakenya ushuru wa juu ilhali umaskini unaua Wakenya wengi.

Muhtasari
  • Kigame alisikitika kwamba ukabila ulikuwa umekita mizizi serikalini haswa chini ya Rais William Ruto ambapo uteuzi uliegemea makabila.
  • Alisema mara tu ufisadi utakapokomeshwa serikali itakuwa na rasilimali za kutosha kuwahudumia Wakenya.
Image: MATHEWS NDANYI

Aliyekuwa mgombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2022 Reuben Kigame ametaka kiongozi wa Azimio la Umoja – One Kenya Raila odinga kuachana na ajenda ya kugawanya nchi ya Kenya.

Kigame alisema pendekezo la hivi majuzi la Odinga la kugawanya nchi lilikuwa la ubinafsi na hatari na pia chini ya kiwango chake cha kiongozi.

"Kama waziri mkuu wa zamani wa nchi hii Odinga anafaa kutetea umoja wa kitaifa na sio kukoma," Kigame alisema.

Kigame alisema licha ya tofauti za kisiasa nchini na Wazee na Wakenya lazima wajilinde dhidi ya migawanyiko na ukabila.

Kigame alihutubia kikao cha wanahabari kando ya barabara mjini Eldoret ambapo alisifu jukumu lililotekelezwa na wapigania uhuru na wale wote waliopoteza maisha wakati wakipigania kuikomboa nchi kutoka kwa maovu mbali mbali ikiwemo dhuluma katika uchaguzi.

Kigame alisikitika kwamba ukabila ulikuwa umekita mizizi serikalini haswa chini ya Rais William Ruto ambapo uteuzi uliegemea makabila.

Wakati uo huo Kigame alimtaka Rais Ruto kuzingatia usalama wa chakula kwa nchi na wala sio miradi ya makazi.

Alisema haikuwa busara kwa Rais kuwalazimisha Wakenya ushuru wa juu ilhali umaskini unaua Wakenya wengi.

"Ukiwauliza Wakenya kipaumbele chao ni chakula na sio nyumba. Watu wakishakula watafanya kazi kwa bidii na kujenga nyumba zao," Kigame alisema.

Kigane alisema baadhi ya kodi zinazoanzishwa zitakuwa mzigo kwa wakulima wakati huu ambapo nchi inakabiliwa na tatizo la chakula.

"Mnadai kuwapa wakulima ruzuku ya mbolea lakini mnaingiza kodi kwenye matrekta na mafuta. Mnatoa kwa mkono mmoja na kuchukua na mwingine", alisema Kigame.

Kigame alisema Rais Ruto anafaa kukabiliana na kuziba mianya ya ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za serikali badala ya kuongeza mapato.

Alisema mara tu ufisadi utakapokomeshwa serikali itakuwa na rasilimali za kutosha kuwahudumia Wakenya.