CS Kuria: Magavana ndio wamiliki wa mradi wa nyumba, sio Serikali ya Kitaifa

Kuria alisisitiza kuwa magavana 47 watakabidhiwa joho la kusimamia utekelezwaji wa mradi huo.

Muhtasari
  • Kwa hivyo, Waziri huyo aliwataka Wakenya kuungana kuunga mkono mradi wa Nyumba na kuzingatia misimamo ya kisiasa.
  • "Mazungumzo hayana hoja, serikali sio mmiliki wa mpango huu, unaenda kutekelezwa katika kaunti," Kuria alisema.
Waziri wa Biashara Moses Kuria
Image: MAKTABA

Waziri wa Biashara Moses Kuria anasema mpango tata wa Nyumba za bei nafuu ni mradi ambao utaongozwa na serikali za kaunti na sio lazima serikali ya kitaifa.

Akiongea Jumatano usiku wakati wa mdahalo wa Grand Conversation ulioandaliwa na Citizen TV, CS Kuria alieleza kuwa kipindi hicho ambacho kimekuwa mjadala wa kitaifa kitatekelezwa katika vitengo vya ugatuzi.

Kuria alisisitiza kuwa magavana 47 watakabidhiwa joho la kusimamia utekelezwaji wa mradi huo.

"Mazungumzo hayana hoja, serikali sio mmiliki wa mpango huu, unaenda kutekelezwa katika kaunti," Kuria alisema.

"Kwa hakika ni magavana 47 ambao ndio wamiliki wa mpango huo kwa sababu tutakuwa na kaunti zote zilizotengewa ardhi na miradi ya nyumba za bei nafuu katika pembe zote za nchi bila kujali ushawishi wa kisiasa."

Huku akitoa mfano wa ziara ya hivi majuzi ya Rais William Ruto katika Kaunti ya Homa Bay, Kuria alisisitiza kuwa mpango huo unanuiwa kuboresha maisha ya Wakenya wote na unapaswa kukaribishwa na wote.

“Nyie kama vyombo vya habari muwaulize wakuu wa mikoa ikiwa wanataka ajira kwa watu wao au la, waulizeni kama hawataki vijana wao wapate ajira, kwa mafundi seremala, wajenzi, hivi katika eneo lenu hamna watu wanaoishi katika vitongoji duni? " Aliweka pozi.

Kwa hivyo, Waziri huyo aliwataka Wakenya kuungana kuunga mkono mradi wa Nyumba na kuzingatia misimamo ya kisiasa.

Mashirika kadhaa wamejitokeza na kupinga mradi huo huku utawa wa Kenya Kwanza ukitetea mradi huo na kueleza kwa kina jnsi Wakenya watasaidika.