Kumpoteza mume ni tukio la kutisha-Ujumbe wa Gavana Wavinya wenye hisia kwa wajane

Mmoja wa viongozi ambao wameadhimisha siku hiyo ni gavana wa kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti.

Muhtasari
  • Ndeti ambaye alifiwa na Mume wake mwaka wa 2016 alitoa ushuhuda kuwa kuwa mjane ni kazi ngumu na inatisha akibainisha kuwa ni hafla ambayo hakuna mtu anayeweza kujiandaa nayo.
GAVANA WA KAUNTI YA MACHAKOS WAVINYA NDETI
Image: KWA HISANI

Wajane kote ulimwenguni leo Ijumaa, Juni 23 wanaadhimisha siku yao maalum inayojulikana kama Siku ya Kimataifa ya Wajane.

Siku ya Kimataifa ya Wajane huadhimishwa kila mwaka na ni siku ya utekelezaji iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa ili kukabiliana na umaskini na ukosefu wa haki unaowakabili mamilioni ya wajane na watu wanaowategemea katika nchi nyingi.

Nchini Kenya, viongozi wanawake kutoka sehemu mbalimbali za Kisiasa walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii kusherehekea siku hiyo huku wakiwatia moyo wajane nchini.

Mmoja wa viongozi ambao wameadhimisha siku hiyo ni gavana wa kaunti ya Machakos Wavinya Ndeti.

kwa kuzingatia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii, Ndeti ambaye pia ni mjane alikiri changamoto zinazowakabili wajane hao.

Ndeti alibainisha kuwa kupoteza mume hubadilisha maisha ya mtu kabisa, hata hivyo, aliwapongeza wajane hao kwa kusimama kidete na kuhakikisha familia zao zinakuwa shwari licha ya kutokuwepo kwa waume zao.

''Hafla ya Siku ya Kimataifa ya Wajane inatukumbusha kuwa maisha ni ya kupita. Nawapongeza wajane wote ambao ni kielelezo cha nguvu, wakiziweka familia zao pamoja baada ya kufariki kwa waume zao." Alichapisha kwenye kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.

Ndeti ambaye alifiwa na Mume wake mwaka wa 2016 alitoa ushuhuda kuwa kuwa mjane ni kazi ngumu na inatisha akibainisha kuwa ni hafla ambayo hakuna mtu anayeweza kujiandaa nayo.

"Naweza kushuhudia kwamba, kufiwa na mume ni tukio chungu, la kutisha ambalo hakuna mtu anayeweza kujiandaa kwa kweli. Kifo cha mwenzi wa ndoa hubadilisha kabisa ulimwengu mzima wa mtu." Alisema.

"Tunatuma salamu za furaha Siku ya Kimataifa ya Wajane kwa wajane wote wa ajabu katika Kaunti ya Machakos na kote ulimwenguni." Aliongeza.

Mume wa gavana aliyetambulika kama Henry Oduwole alifariki mwaka wa 2016 katika hospitali ya Nairobi baada ya kulazwa akiwa na shinikizo la damu.

Kutoka kwetu wanajambo tunawatakia wajane wote siku njema wanaposherehekea siku hii maalum kwao.