Ruto aongoza nchi kwa maombolezo ya waathiriwa wa ajali Londiani

Rais alisema inatia wasiwasi kuwa baadhi ya waliofariki katika ajali hiyo walikuwa ni vijana wadogo wenye ahadi kubwa ya maisha.

Muhtasari

Kulikuwa na hofu kwamba idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka hadi 55, kwani baadhi ya miili ilisalia kwenye mabaki.

RAIS WILLIAM RUTO
Image: TWITTER

Rais William Ruto amewaongoza wakenya kuomboleza kifo cha watu 45 kwenye ajali mbaya ya barabarani eneo la Londiani, kando ya barabara kuu ya Nakuru-Kericho.

Kulikuwa na hofu kwamba idadi ya waliokufa inaweza kuongezeka hadi 55, kwani baadhi ya miili ilisalia kwenye mabaki.

 

Rais alisema inatia wasiwasi kuwa baadhi ya waliofariki katika ajali hiyo walikuwa ni vijana wadogo wenye ahadi kubwa ya maisha.

Ruto alitoa wito kwa madereva kuendesha magari kwa uangalifu wakati huu wa mvua na kuwatakia wale waliopata majeraha kupona kwa haraka.

"Nchi inaomboleza pamoja na familia ambazo zimepoteza wapendwa wao katika ajali mbaya ya barabarani eneo la Londiani, Kaunti ya Kericho. Inasikitisha kwamba baadhi ya walioaga dunia ni vijana wenye maisha marefu ya siku za usoni na wafanyabiashara waliokuwa kwenye shughuli zao za kila siku.

 

"Tunawaombea afueni ya haraka manusura wote; mko katika mawazo yetu. Tunawaomba madereva wa magari kuwa waangalifu zaidi barabarani, hasa wakati huu tunapokumbwa na mvua kubwa," rais alisema kwenye taarifa.

 

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia alisema inasikitisha kwamba nchi imepoteza watu wengi katika ajali moja.

 

Waziri Mkuu huyo wa zamani aliwataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuwa waangalifu zaidi.

 

"Hii ni siku ya huzuni kwa nchi yetu ... kwani watoto wengi wamekuwa mayatima na wengi wajane... Kwa waliojeruhiwa, tunawatakia ahueni ya haraka," Raila alisema.

 

Naibu Rais Rigathi Gachagua pia alisema ajali hiyo mbaya ya barabarani inaleta hasara isiyoelezeka kwa taifa letu.

Aliongeza kuwa ni uchungu kupoteza wapendwa wako katika umri wowote hasa katika ajali mbaya ya barabarani namna hii.

 

"Mawazo na dua zetu zipo kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kupona haraka manusura wa ajali hii mbaya ya barabarani. Naomba umakini wa hali ya juu katika barabara zetu wakati wote kwa watumiaji wote wa barabara."