Breki zilifeli-Dereva wa lori lililoua zaidi ya watu 50 Londiani hatimaye azungumza

Anasema kuwa lori hilo lilikuwa likisafirisha shehena nzito ya mifuko ya saruji hadi Uganda kupitia mpaka wa Busia.

Muhtasari
  • Dereva huyo ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, alisema ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu ya breki na kusababisha lori hilo kushindwa kulidhibiti.
Ajali ya Londiani.
Ajali ya Londiani.
Image: HISANI

Dereva wa lori aliyehusika katika ajali ya Londiani iliyosababisha vifo vya takriban watu 50 amezungumza kwa mara ya kwanza, akitoa maelezo ya kilichojiri siku hiyo ya maafa.

Dereva huyo ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru, alisema ajali hiyo ilisababishwa na hitilafu ya breki na kusababisha lori hilo kushindwa kulidhibiti.

“Nilitoka katika Kiwanda cha Saruji cha Simba cha Salgaa nikielekea Uganda kupitia Busia na kushindwa kulidhibiti lori langu kutokana na hitilafu ya breki. Nilikuwa na dereva mwenzangu na sijui kama amelazwa," alisema.

Anasema kuwa lori hilo lilikuwa likisafirisha shehena nzito ya mifuko ya saruji hadi Uganda kupitia mpaka wa Busia.

Majeruhi waliojeruhiwa katika ajali hiyo pia wamelazwa katika hospitali hiyo, ambapo daktari aliyekuwa akiwahudumia alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya wahasiriwa.

“Kati ya hao walikuwa wanawake watatu na wanaume sita, wanawake watatu wamejeruhiwa zaidi sehemu za chini za miguu, kati ya wanaume sita walikuwapo wawili waliojeruhiwa kichwani na kisha wengine wanne wamejeruhiwa hasa kichwani na sehemu ya chini ya miguu na tumbo,” daktari alisema.

"Wanawake watatu wamefanyiwa upasuaji na wako sawa ingawa bado hawajaruhusiwa. Miongoni mwa wale wanaume sita mmoja wao alikufa,” Aliongeza.