Mwanafunzi wa kidato cha nne akiri mauaji ya msichana wa miaka 17 Naivasha

Muda mfupi baadaye, mshukiwa alitembea hadi kituo cha polisi cha eneo hilo kukiri mauaji hayo.

Muhtasari
  • Mwili ulikuwa umekatwa sana kichwani, waya mwembamba shingoni na kamba za viatu miguuni.

Maafisa wa upelelezi wanamshikilia mwanafunzi wa kidato cha nne kuhusiana na mauaji ya msichana ambaye mwili wake ulipatikana umetupwa kando ya barabara huko Naivasha.

Polisi walisema mshukiwa alikiri mauaji ya Brenda Bosibori, 17, ambaye mwili wake ulipatikana mnamo Julai 2 katika eneo la Karagita.

Mwili ulikuwa umekatwa sana kichwani, waya mwembamba shingoni na kamba za viatu miguuni.

Damu pia zilikuwa zikimtoka mdomoni na masikioni wakati polisi walipofika na kuuchukua mwili huo.

Muda mfupi baadaye, mshukiwa alitembea hadi kituo cha polisi cha eneo hilo kukiri mauaji hayo.

Alikuwa ameenda kituoni kuripoti mauaji hayo, polisi walisema.

Aliwaambia polisi kwamba alimchukua marehemu kutoka nyumbani kwa wazazi wake na kumpeleka nyumbani kwao ambapo alimfungia chumbani kwake na kumnyonga kwa kutumia kamba za viatu.

Kisha akauficha mwili wake chumbani mwake hadi usiku wa manane, akauburuta na kuutupa kando ya barabara.

Mshukiwa aliwaambia polisi alirudi nyumbani kwa mamake na akalala hadi siku iliyofuata.

Mama wa msichana aliyekufa aliwaambia polisi kwamba mshukiwa pia alimpigia simu mapema.

Alisema binti huyo alipopotea, alikuwa amempa pesa ya kifungua kinywa kabla ya kwenda kazini.

Alisema mshukiwa pia aliwarudishia funguo ya nyumba akisema marehemu aliwacha kwake.

Ilibainika kuwa mshukiwa alikuwa ameenda nyumbani kwa Brenda mapema siku hiyo kusaidia kazi za nyumbani, ikiwa ni pamoja na kuosha vyombo.

Wawili hao kisha waliondoka nyumbani pamoja na inaonekana ilikuwa mara ya mwisho kwa msichana huyo kuonekana akiwa hai.

Rose aliwaambia polisi alipomwambia mshukiwa kwamba binti yake hayupo, alionekana kushtuka na akajitolea kusaidia upekuzi.

Na kwa takriban saa saba, mama huyo na mshukiwa pamoja na wenyeji wengine walizunguka eneo hilo wakimtafuta msichana aliyetoweka bila mafanikio.

Mshukiwa huyo hata alimtaka mwanamke huyo aende nyumbani na kupumzika hadi siku iliyofuata rafiki yake alipompigia simu akisema mwili wa msichana huyo ulikuwa umepatikana katika eneo hilo.

Naibu afisa wa polisi wa Naivasha, Samuel Kiplong alisema wanashuku mshukiwa na msichana aliyefariki walitofautiana kuhusu mapenzi na pesa.

Alisema wanachunguza kesi ya mauaji.

"Tunashuku kuwa kisa cha mapenzi kilizidi kuwa mbaya. Mshukiwa pia anadai alikuwa amempa msichana huyo Sh200 kwa sababu zisizoeleweka,” akasema.

Polisi walimpeleka mshukiwa mahakamani ambapo walitaka siku zaidi kukamilisha uchunguzi wao kuhusu mauaji hayo.