Twitter yatishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya programu ya Threads

Mwonekano na hisia za Threads ni sawa na zile za Twitter, mwandishi wa masuala ya teknolojia wa BBC James Clayton alibainisha.

Muhtasari

• Mwonekano na hisia za Threads ni sawa na zile za Twitter, mwandishi wa masuala ya teknolojia wa BBC James Clayton alibainisha. Alisema upashaji wa habari na utumaji upya ni wa kawaida sana.

• Zaidi ya watu milioni 30 wamejisajiri kwenye programu hiyo mpya, kulingana na Meta.

Twitter inaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Meta kuhusu programu yake pinzani inayokua kwa kasi ya Threads.

Threads, ambayo ilizinduliwa kwa usajili wa mamilioni ya watu siku ya Jumatano, ni sawa na Twitter na imeanzishwa na wakuu wa Meta kama programu mbadala "rafiki".

Mmiliki wa Twitter Elon Musk na Kampuni yake walisema "ushindani ni sawa, kudanganya sio" - lakini Meta ilikanusha madai katika barua ya kisheria kwamba wafanyakazi wa zamani wa Twitter walisaidia kuunda programu ya Threads.

Zaidi ya watu milioni 30 wamejisajiri kwenye programu hiyo mpya, kulingana na Meta.

Mwonekano na hisia za Threads ni sawa na zile za Twitter, mwandishi wa masuala ya teknolojia wa BBC James Clayton alibainisha. Alisema upashaji wa habari na utumaji upya ni wa kawaida sana.

Katika hatua iliyoripotiwa kwanza na chombo cha habari cha Semafor, wakili wa Twitter Alex Spiro alituma barua kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Meta Mark Zuckerberg Jumatano akiishutumu Meta kwa "utumiaji mbaya wa kimfumo, wa makusudi, na usio halali wa siri za biashara za Twitter na mali nyingine za kiakili"- katika kuunda Threads.

Bw Spiro hasa alidai kuwa Meta ilikuwa imeajiri wafanyakazi kadhaa wa zamani wa Twitter ambao "walikuwa na wanaendelea kupata siri za kibiashara za Twitter na taarifa nyingine za siri sana" ambazo hatimaye ziliisaidia Meta kuunda kile alichokiita programu ya "kunakili" Threads.

"Twitter inakusudia kutekeleza kwa dhati haki zake za uvumbuzi, na inaitaka Meta kuchukua hatua za haraka kuacha kutumia siri zozote za biashara za Twitter au habari nyingine za siri," barua hiyo inasema.

BBC, imeona nakala ya barua hiyo, ambayo imewasiliana na Meta na Twitter kwa maoni.

Bw Musk alisema kuwa "ushindani ni sawa, kudanganya sio" akijibu chapisho kwenye Twitter ambalo lilirejelea barua ya kisheria.