Hatutaruhusu hasara zaidi kutokana na maandamano-Kindiki kwa Azimio

Waandamanaji Jumatano waliondoa kizuizi cha Expressway karibu na Mlolongo.

Muhtasari
  • Waziri huyo ambaye alikuwa Narok alitaja maandamano ya Jumatano kama machafuko na uhujumu uchumi.
Waziri wa Mambo ya Ndani Prof. Kithure Kindiki
Image: TWITTER

Waziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa Kithure Kindiki amezungumza vikali kuhusu maonyesho ya siku tatu yaliyopangwa na Azimio la Umoja.

Kindiki alisema wizara yake haitaruhusu hasara yoyote zaidi kutokana na maandamano yanayoongozwa na muungano wa Azmio.

"Ujeuri, kiherehere na ujuaji umejaa Kenya hii…msijaribu kuandamana wiki ijayo," alisema.

Waziri huyo ambaye alikuwa Narok alitaja maandamano ya Jumatano kama machafuko na uhujumu uchumi.

"Haki zako zinaishia pale ambapo haki za watu wengine zinaanzia. Hakuna haki au uhuru wa kupora, kuua, kujeruhi au kuharibu mali ya kibinafsi na ya umma. Hatutaruhusu tena wiki ijayo," aliongeza.

Waziri huyo alihoji zaidi nia ya watu hao kubomoa na kuharibu samani za barabarani na kupora mali.

"Je, kufunga barabara, kuharibu barabara ya mwendokasi, kupiga mawe na kujeruhi maafisa wa usalama, kupora mali ya kibinafsi na ya umma kunapunguzaje gharama ya maisha?" Kindiki aliuliza.

Waandamanaji Jumatano waliondoa kizuizi cha Expressway karibu na Mlolongo.

Walionekana wakivuta kizuizi kwa nguvu ili kukiondoa.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alisema kuwa uharibifu uliofanywa kwenye Barabara ya Nairobi Expressway unaweza kuwa zaidi ya Sh700 milioni.

Hata hivyo muungano wa Azimio ulisema kwamba utafanya maandamano ya siku tatu wiki ijayo.