Watu 2 wamefariki na 52 kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Barabara kuu ya Nairobi - Nakuru

Polisi walisema kasisi mmoja na mkewe walifariki papo hapo baada ya trela lililokuwa na hitilafu ya breki kugonga gari lao katika ajali hiyo ambapo magari 20 yalihusika.

Muhtasari

• Miongoni mwa waliojeruhiwa ni wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Twilight iliyoko Kayole, Kaunti ya Nairobi.

•  Polisi walisema wanafunzi hao walikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya PCEA Kikuyu.

 

Crime Scene
Image: HISANI

Takriban watu wawili walifariki huku makumi ya wengine wakijeruhiwa kufuatia ajali ya barabarani eneo la Muguga kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru Ijumaa usiku.

Polisi walisema kasisi mmoja na mkewe walifariki papo hapo baada ya trela lililokuwa na hitilafu ya breki kugonga gari lao katika ajali hiyo ambapo magari 20 yalihusika, likiwemo basi la shule lililokuwa na wanafunzi 44.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari ya Twilight iliyoko Kayole, Kaunti ya Nairobi.

Polisi walisema wanafunzi hao walikimbizwa na kulazwa katika Hospitali ya PCEA Kikuyu.

Kamanda wa Polisi wa kaunti ndogo ya Kikuyu Ronald Kirui alisema wengine wengi waliojeruhiwa walipelekwa hospitalini.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Aliwaambia madereva kudumisha nidhamu ya udereva na kuhudumia magari yao ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na ajali hizo.

Wenyeji walizitaka mamlaka husika zinazoongozwa na KeNHA kukamilisha sehemu ya barabara ambapo njia za kutoa huduma zitajengwa ili kuepusha hasara zaidi ya maisha.

Visa vya ajali mbaya vimeongezeka licha ya kampeni za kukabiliana na tishio hilo.