Hili ni taifa ambalo limetekwa,tumerejea enzi za Moi-Seneta Madzayo

Madzayo alisema miswada inalazimishwa kushushwa kooni na Wakenya bila mjadala mkubwa ambao umekuwa ukiendeshwa na wabunge bungeni.

Muhtasari
  • Alisema sasa Wakenya wanapaswa kuwa waangalifu kila wanapozungumza hadharani kwani hawajui ni nani anayeweza kuwasikiliza

Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo sasa anadai kuwa nchi inarejea enzi za utawala wa Moi ambapo Rais wa zamani alitawala kwa mkono wa chuma.

Alisema sasa Wakenya wanapaswa kuwa waangalifu kila wanapozungumza hadharani kwani hawajui ni nani anayeweza kuwasikiliza

"Tumerejea enzi za  Moi kila Mkenya alipokuwa akiongea, ilibidi waangalie nyuma ya bega lao kuona ikiwa kuna mtu mwingine anayesikiliza," alisema.

Alisema demokrasia ya Kenya iko hatarini kwa vile uhuru wa kujieleza unakabiliwa na tishio.

"Hatufanani tena na nchi huru. Hili ni taifa ambalo limetekwa."

Zaidi, alidai kuwa bunge limezibwa.

Madzayo alisema miswada inalazimishwa kushushwa kooni na Wakenya bila mjadala mkubwa ambao umekuwa ukiendeshwa na wabunge bungeni.

“Nawaomba wale watu wanaotawala madaraka sasa, kuna kesho na mabadiliko ya uongozi,” alisema.

Aliongeza kuwa viongozi wa sasa hawatataka kuona wanachofanya kwa wengine wanafanyiwa.

Haya yanajiri huku serikali ikielekea kuchukua hatua kali dhidi ya baadhi ya viongozi wa Azimio.

Matamshi yake yanajiri wakati ambapo upinzani na Serikali zimekabana kooni, kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Kwa muda sasa upinzani umekuwa ukiandaa maandamano kupinga serikali ya Ruto.

Ni maandamano ambayo yameshuhudia baadhi ya wabunge wa muungano wa Azimio kukamatwa.

Mmoja wa wabunge waliokamatwa ni Babu Owino ambaye alifikishwa katika mahakama ya Milimani siku ya Ijumaa na kuachiliwa kwa dhamana.

Hakimu mkuu wa Milimani Lukas Onyina katika uamuzi wake Ijumaa asubuhi alibainisha kuwa shtaka dhidi ya washtakiwa linaweza kuadhibiwa wakipatikana na hatia kwa kifungo cha miaka saba gerezani.

Hata hivyo, alisema upande wa mashtaka haujabainisha ni nani kati ya washtakiwa hao ataingilia mashahidi.

"Uchunguzi kamili wa hati ya kiapo hauonyeshi sababu za msingi za kuwanyima dhamana washtakiwa. Kila mmoja wa washtakiwa anapewa bondi ya Sh200,000 na dhamana ya fedha taslimu Shilingi 100,000," aliamuru hakimu.

Pia walioachiliwa kwa bondi ni Tom Odondo, Michael Otieno, Pascal Ouma, Kevin Wambo na Willys Owino.

Siku ya Alhamisi, Babu Owino na Gaucho walikanusha njama ya kutekeleza shughuli za uasi ambazo zinaathiri utulivu wa umma.