Wanga awaongoza viongozi wa Nyanza kufanya mkesha kwa wahanga wa maandamano

Olala alisema haki ya kuandamana imetolewa kwenye katiba na hivyo polisi lazima waheshimu katiba.

Muhtasari
  • Wanga na viongozi wengine wa eneo hilo waliokuwa wakizungumza wakati wa hafla hiyo katika Kisiwa cha Rusinga, eneo bunge la Suba Kaskazini wamelaani ukatili wa polisi
Wanga awaongoza viongozi wa Nyanza kufanya mkesha kwa wahanga wa maandamano
Image: TWITTER

Viongozi kutoka eneo la Nyanza wameungana na wakaazi kufanya mikesha kwa watu waliouawa wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

Katika Kaunti ya Homa Bay, Gavana Gladys Wanga aliongoza viongozi na wafuasi wa Azimio kuwasha mishumaa kuwakumbuka waathiriwa wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano.

Wanga na viongozi wengine wa eneo hilo waliokuwa wakizungumza wakati wa hafla hiyo katika Kisiwa cha Rusinga, eneo bunge la Suba Kaskazini wamelaani ukatili wa polisi, ambao uliwaacha Wakenya wengine wakiwa wamekufa, na wengine kuuguza majeraha ya risasi.

Aliandamana na naibu wake Oyugi Magwanga, Spika wa Bunge la Kaunti Julius Gaya, na waliahidi kusimama na wakazi wakikabiliana na bili za hospitali.

Katika Kaunti ya Migori, wakaazi waliungana na Wakenya wengine katika mkesha huo wa ukumbusho, wakiongozwa na viongozi wa chama cha ODM kutoka eneo hilo.

Walifanya vikao vifupi vya maombi katika uwanja wa Posta, ambapo katibu mkuu wa chama cha ODM Joseph Olala aliwataka polisi kukoma kuwaua watu wasio na hatia wakati wa maandamano.

Olala alisema haki ya kuandamana imetolewa kwenye katiba na hivyo polisi lazima waheshimu katiba.

Matamshi sawa na hayo yaliungwa mkono na kiongozi wa vijana wa ODM kaunti ya Migori Erick Opany na mwenyekiti wa Bunge la Wananchi kaunti ya Migori Charles Osewe walioomba mamlaka husika kuwachukulia hatua maafisa wa polisi waliowaua na kuwajeruhi waandamanaji kwa amani.

Viongozi Wa Nyanza Wafanya Mkesha Kwa Wahanga Wa Maandamano Ya Kupinga Serikali