Alikuwa ana fadhili maandamano ya Azimio-Wambugu,Cherargei wasema baada ya Uhuru kuungana na Azimio

Seneta huyo alimthubutu Rais huyo wa zamani kuwania urais mwaka wa 2027.

Muhtasari
  • Ikumbukwe kuwa viongozi wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wamekuwa kwenye rekodi wakimtuhumu Rais huyo wa zamani kwa kufadhili maandamano ya Azimio.
(KUSHOTO)KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA,(KATI) RAIS MSTAAFU UHURU KENYATTA,(KULIA) KIONGOZI WA WACHACHE KATIKA BUNGE OPIYO WANDAYI
Image: RADIOJAMBO

Aliyekuwa Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu na seneta Cherargei wamevunja ukimya baada ya aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria misa ya kuwaombea waliojeruhiwa na polisi kwenye maandamano na kuwaenzi waliouawa iliyoandaliwa na muungano wa Azimio.

Akitumia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Ngunjiri alisema kuwa sasa anaweza kuamini kuwa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta amekuwa akifadhili maandamano ya Azimio.

Ikumbukwe kuwa viongozi wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wamekuwa kwenye rekodi wakimtuhumu Rais huyo wa zamani kwa kufadhili maandamano ya Azimio.

"Kwa kweli, sasa naweza kuamini kwamba alikuwa akifadhili maadamano," Ngunjiri alisema baada ya Rais huyo wa zamani kufika katika kituo cha SKM kwa ajili ya misa ya mahitaji iliyoandaliwa na Azimio kwa heshima ya waliopoteza maisha wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

Kwa upande wake Cherargei amesema kuwa;

"Tuliposema Uhuru ndiye mfadhili mkuu wa Tinga/Azimio-OKA Maandamos & uhujumu uchumi pamoja na nia ya kuipindua serikali iliyochaguliwa na Mungu, marafiki wengi waliikataa. HATIMAYE amejitokeza kuangalia ufadhili wake na kusherehekea damu ya Wakenya waliofariki katika harakati zao za kusaka madaraka/handcheque/handshake.

Moi na kibaki walipostaafu walistaafu kwa mujibu wa Sheria ya Mafao ya Kustaafu ya Rais tofauti na Uhuru ambaye anataka kuwa na keki yake na kuila.

Sheria inasema ili mradi Uhuru yuko  sawa kisiasa hawezi kupata mafao ya Rais ya kustaafu iwe hivyo!.

Seneta huyo alimthubutu Rais huyo wa zamani kuwania urais mwaka wa 2027.

"Ikiwa Uhuru ni mwanamume vya kutosha kwa nini asiwanie urais tena 2027 ?"