Viongozi wa Azimio watoa zaidi ya milioni 4 kwa waathiriwa wa maandamano

"Nataka kutambua kwa shukrani za dhati mchango wa ndugu yetu Uhuru Kenyatta wa shilingi milioni 1, na wa ndugu yetu Raila Odinga wa shilingi milioni 1, nmi natoa shilingi nusu milioni," Kalonzo alisema.

Muhtasari

• Akiongea katika kituo cha SKM jijini Nairobi, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema wamezindua Citizen Emergency Fund ili kusaidia waathiriwa

• Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alisema wabunge wametoa shilingi milioni 1.5 kwa waathiriwa.

Viongozi wa Azimio Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Rais msattafu Uhuru Kenyatta wakati wa maombi yaliyoandaliwa na muungano huo huko Karen, July 28, 2023.
Viongozi wa Azimio Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Rais msattafu Uhuru Kenyatta wakati wa maombi yaliyoandaliwa na muungano huo huko Karen, July 28, 2023.
Image: ENOS TECHE

Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, Kinara wa Upinzani Raila Odinga na viongozi wengine wa Azimio wametoa zaidi ya shilingi milioni 4 kwa hazina iliyobuniwa kusaidia wahanga wa wa maandamano ya kupinga serikali.

Akiongea katika kituo cha SKM jijini Nairobi, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisema wamezindua hazina ya Citizen Emergency Fund ili kusaidia waathiriwa.

"Hata tunapoendelea kuomboleza na kuwaombea waathiriwa, tumeamua kuzindua hazina ya dharura ya raia ili kutoa msaada kwa familia za waliokufa na waliojeruhiwa," Kalonzo alisema.

Kalonzo aliwashukuru rais mustaafu Uhuru Kenyatta na kinara wa Azimio Raila Odinga kwa kuchangia hazina hiyo kwa kima cha shilingi milioni moja kila mmoja huku Kalonzo akitoa shilingi laki tano.

"Nataka kutambua kwa shukrani za dhati mchango wa ndugu yetu Uhuru Kenyatta wa shilingi milioni 1, na wa ndugu yetu Raila Odinga wa shilingi milioni 1, mimi natoa shilingi nusu milioni," Kalonzo alisema.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi alisema wabunge wametoa shilingi milioni 1.5 kwa waathiriwa.

Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa aliahidi kutoa shilingi 200,000 kwa hazina hiyo.

Kalonzo alitoa wito kwa Wakenya kuendelea kutia sahihi zao kwenye tovuti ya 'Tumechoka' akisema watu milioni 8.2 walikuwa wametia saini kufikia siku ya Ijumaa.

"Tunapozungumza saini kufikia leo zinafikia milioni 8.2 na bado tunahesabu. Tafadhali endelea kutia saini na uwe jasiri na usimame imara,"

Viongozi hao walikuwa wamehudhuria ibada katika kituo cha SKM huko Karen Nairobi kwa heshima ya waathiriwa wa maandamano. 

Viongozi wa Azimio wakiongozwa na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga walihudhuria.

Muungano wa Azimio uliitisha maandamano hayo kwa maombi ya kuwakumbuka wahanga wa maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha. 

Makasisi waliongoza ibada ya maombi na kulaani kile walichokiita kuwaua raia wasio na hatia.