Safaricom imeongeza ada ya malipo ya M-Pesa kuanzia leo Julai 29

Kando na M-Pesa, Safaricom pia watafanya mabadiliko katika bei za vifurishi kama kwa kupiga simu, SMS, intaneti ya Fibre na deta ya bando.

Muhtasari

• Kupitia notisi ambayo imeonekana na Radiojambo.co.ke, Safaricom walitangaza kwamba bei mpya zitaanza kufanya kazi Julai 29.

• Ada ya kutozwa mtu anapofanya biashara kupitia namba ya Till itaongezeka kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia 0.55

Tawi la Two Riverws litafungwa mwisho Agosti 32 mwaka 2022.
Duka la Safaricom Tawi la Two Riverws litafungwa mwisho Agosti 32 mwaka 2022.
Image: Facebook

Wakenya wameshauriwa kukaza mikanda yao huku hali ngumu ya uchumi ikizidi kung’ata kila sekta.

Ya hivi karibuni imekuwa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kutangaza kupandisha gharama za vifurishi vyao, saa chache tu baada ya mahakama ya rufaa kuondoa agizo lililokuwa limesitishwa kutekelezwa kwa sheria ya fedha ya 2023 iliyotiwa saini na rais Ruto mwezi mmoja uliopita.

Kupitia notisi ambayo imeonekana na Radiojambo.co.ke, Safaricom walitangaza kwamba bei mpya zitaanza kufanya kazi Julai 29 ambayo ni leo Jumamosi.

Mabadiliko haya yatang’ata kila upande unaotegemea huduma za Safaricom kutoka mawasiliano hadi biashara.

Ada ya kutozwa mtu anapofanya biashara kupitia namba ya Till itaongezeka kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia 0.55, katika kile kamuni hiyo ilisema ni hatua ya kuendana na ongezeko la kiwango cha ushuru kilichopendekezwa kwenye mswada wa fedha uliotiwa sahihi na rais kuwa sheria mwezi uliopita.

“Kufuatia kupitishwa kwa mswada wa fedha wa 2023 kuwa sheria, na kuondolewa kwa agizo la kuzuia kutekelezwa kwa sheria hiyo na mahakama ya rufaa Julai 28, kuanzia Julai 28, tutafanya mabadiliko katika huduma zetu za SMS, kupiga simu, MPESA, bando na intaneti ya Fibre ili kuendana na ongezeko la kiwango cha ushuru kutoka 12% hadi 15%,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Safaricom pia ilisema kuwa imekagua gharama zake za data, nyuzi, simu na Huduma ya Ujumbe Mfupi (SMS). Hii ilifuatia kupungua kwa ushuru wa bidhaa kutoka 20% hadi 15%.