Azimio kutangaza mwongozo mpya kuhusu hatima ya maandamano leo Jumapili

Kalonzo alificua hilo Ijumaa wakati wa mkusanyiko wa kucnagisha fedha za kusaidia familia za wale ambao walipatwa na majeraha wakati wa maandamano ya kupinga ushuru uliopendekezwa na serikali.

Muhtasari

• Kinara wa Azimio Raila Odinga na Kenyatta, ambao wote hawakuzungumza katika hafla hiyo, kila mmoja alitoa Ksh.1 milioni kwa hazina ya familia za waathiriwa.

• Kalonzo alichangia Ksh.500,000, Eugene Wamalawa Ksh.200,000, huku Wabunge wa Azimio kwa pamoja wakichangia Ksh.1.5 milioni.

Viongozi wa Azimio Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Rais msattafu Uhuru Kenyatta wakati wa maombi yaliyoandaliwa na muungano huo huko Karen, July 28, 2023.
Viongozi wa Azimio Kalonzo Musyoka, Raila Odinga na Rais msattafu Uhuru Kenyatta wakati wa maombi yaliyoandaliwa na muungano huo huko Karen, July 28, 2023.
Image: ENOS TECHE

Mrengo wa upinzani, Azimio la Umoja One Kenya sasa wamesema kwamba kesho Jumapili watatoa mwongozo mpya kuhusu hatima ya maandamano ya kupinga ushuru uliopendekezwa na serikali ya Kenya Kwanza.

Azimio walitangaza hayo Ijumaa katika Kituo cha Kamandi cha Stephen Kalonzo Musyoka (SKM) wakati wa ibada ya kuwaomboleza waathiriwa wa visa vya kupigwa risasi na polisi, wakiikashifu serikali ya Rais William Ruto kwa kukosa kukiri mauaji ya kiholela ya waandamanaji.

"Ninataka kutangaza kwa niaba yetu kwamba Jumapili, Julai 30, tutawasiliana na taifa kuhusu hatua yetu inayofuata kuhusu maandamano ya kupinga ushuru," alisema kiongozi wa Wiper Kalonzo katika taarifa ya pamoja.

Kalonzo aliongeza kuwa mrengo wa kisiasa wa upinzani uliazimia kuanzisha hazina ya kusaidia familia za waathiriwa wote wa ukatili wa polisi wakati wa maandamano yaliyosimamishwa dhidi ya serikali.

Sherehe hiyo iliadhimisha kuonekana tena hadharani kwa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliungana na viongozi wa Azimio kuwakumbuka zaidi ya wahasiriwa 30 wa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

Kinara wa Azimio Raila Odinga na Kenyatta, ambao wote hawakuzungumza katika hafla hiyo, kila mmoja alitoa Ksh.1 milioni kwa hazina ya familia za waathiriwa.

Kalonzo alichangia Ksh.500,000, Eugene Wamalawa Ksh.200,000, huku Wabunge wa Azimio kwa pamoja wakichangia Ksh.1.5 milioni.

Kwa jumla, timu ya upinzani ilifanikiwa kukusanya jumla ya Ksh.4.2 milioni.

"Hata tunapoendelea kuomboleza, kusherehekea na kuwaombea waathiriwa, tunaenda mbali zaidi kuzindua Hazina ya Dharura ya Wananchi ili kutoa msaada wa vitendo kwa familia za waliokufa na waliojeruhiwa," Kalonzo alisema.

"Tunawaomba Wakenya wote wenye nia njema, wale wanaopenda haki, wale wanaomngoja Bwana, wawasaidie raia wenzao kwa kuchangia hazina hii."

Magavana katika kaunti za Machakos, Kisii, Homa Bay, Siaya na Migori wote waliondoa bili za hospitali kwa wale wanaouguza majeraha ya risasi na kulazwa katika vituo mbalimbali vya afya katika vitengo vyao vya ugatuzi.