Aliyekuwa kamishna wa IEBC, Roselyn Akombe amkumbuka Chris Msando kwa ujumbe wa kihisia

Akombe alipongeza mchango wa marehemu kwa IEBC na kueleza imani yake kwamba siku moja haki itapatikana.

Muhtasari

•Marehemu Chris Musando alipatikana amefariki mnamo Julai 31, 2017, siku chache tu kabla ya uchaguzi kufanyika.

•Akombe alilalamika kuhusu machungu ya kuona wahusika wa mauaji ya Msando wakiendelea kuwa huru bila kuadhibiwa.

Chris Msando, mkuu wa teknolojia katika tume ya uchaguzi ya Kenya, aliuawa miaka sita iliyopita
Chris Msando, mkuu wa teknolojia katika tume ya uchaguzi ya Kenya, aliuawa miaka sita iliyopita
Image: BBC

Aliyekuwa Kamishna wa tume ya IEBC, Dkt Roselyn Akombe ameadhimisha miaka sita tangu mauaji ya mtaalamu wa teknolojia, marehemu Chris Msando.

Marehemu Chris Msando ambaye alikuwa mkuu wa kitengo cha IT katika Tume ya IEBC kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 alipatikana amefariki mnamo Julai 31, 2017, siku chache tu kabla ya uchaguzi kufanyika. Uchunguzi wa mwili wake ulibaini kuwa aliteswa hadi kufa.

Huku akimkumbuka afisa huyo wake wa zamani siku ya Jumatatu, Dkt Akombe ambaye baadaye alijiuzulu kufuatia kisa hicho cha kuhuzunisha aliibua malalamishi kuhusu machungu ya kuona wahusika wa mauaji hayo wakiendelea kuwa huru bila kuadhibiwa.

“Imepita miaka sita tangu wakutese kikatili na kukuua wewe mfanyakazi wangu, Chris Msando. Wakati mwingine inahisi kuwa si haki kuona waliohusika na mauaji hayo ya kikatili na wawezeshaji wao wakizurura kwa uhuru,” Akombe alisema katika taarifa aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Twitter.

Mtaalamu huyo wa masuala ya kidiplomasia alipongeza mchango wa marehemu kwa IEBC na kueleza imani yake thabiti kwamba siku moja haki itapatikana.

“Lakini tunajua kuwa haki itapatikana siku moja tunapokusherekea kama shujaa wa haki ya uchaguzi na utawala bora. Endelea kupumzika kwa nguvu,” alisema.

Uchunguzi wa maiti uliofanywa baada ya kifo chake ulifichua kuwa afisa huyo wa zamani wa IEBC ambaye mwili wake ulipatikana mwishoni mwa Julai 2017 aliteswa vikali na kunyongwa hadi kufa.

Msando alikuwa na mikwaruzo mirefu na michubuko mgongoni na mikononi, daktari mkuu wa serikali Johansen Oduor alisema.

Bw Msando alikuwa msimamizi wa mfumo wa upigaji kura wa kompyuta wa Kenya kwa uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 2017.

Mwili wake uligunduliwa karibu na maiti ya mwanamke katika msitu viungani mwa jiji la Nairobi wikendi.

“Hakukuwa na shaka kwamba aliteswa na kuuawa,” Wafula Chebukati, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) wa wakati huo, alisema alipokuwa akitangaza kifo chake.