Mazungumzo na Azimio hayahusu kugawana mamlaka - Ruto

Alisema wakati wa siasa za ushindani na nafasi za viongozi ulimalizika katika uchaguzi uliopita.

Muhtasari
  • Gachagua alisema Serikali, chini ya Rais Ruto, iliweka mikakati thabiti inayolenga kubadilisha Kenya.

Rais William Ruto amesema mazungumzo na Upinzani si kuhusu kugawana mamlaka.

Rais alishikilia kuwa mazungumzo hayo yatahusu masuala ya watu.

Alisema wakati wa siasa za ushindani na nafasi za viongozi ulimalizika katika uchaguzi uliopita.

"Kazi iliyo mbele yetu ni kuhusu mahitaji ya watu," alidokeza.

Alizungumza Jumamosi katika siku yake ya kwanza ya ziara ya maendeleo ya Mlima Kenya, akiwahutubia wafanyabiashara na watu wa Githurai, Juja, Kenol, Makuyu, Kambiti, Makutano, Kagio, Baricho na Karatina.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, Mawaziri Moses Kuria, Alice Wahome, Magavana Kimani Wamatangi (Kiambu), Irungu Kangata (Muranga), Anne Waiguru (Kirinyaga) na wabunge wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichungw’ah walihudhuria.

Rais Ruto alisema Serikali itachukua hatua madhubuti dhidi ya majaribio yoyote ya vurugu katika siasa.

Alisema Serikali haitavumilia uharibifu wa mali, uvunjifu wa biashara na kupoteza maisha ya watu.

"Sisi ni nchi ya kidemokrasia ambayo inatii utawala wa sheria," alisema.

Gachagua alisema Serikali, chini ya Rais Ruto, iliweka mikakati thabiti inayolenga kubadilisha Kenya.

“Kazi yetu ni kukuunga mkono ili kufikia malengo haya, na hatutaruhusu mtu yeyote kuwavuruga,” alisema.

Kwa upande wake Mudavadi aliutaka Upinzani kuheshimu demokrasia ya nchi na kuipa serikali nafasi ya kuwatumikia wananchi.