Gavana Natembeya ateuliwa kuwa Naibu Kiongozi wa DAP-K

Chama hicho kinaongozwa na Eugene Wamalwa na Natembeya aliyewania kiti cha ugavana Trans Nzoia kupitia chama hicho.

Muhtasari
  • Alionyesha imani na timu mpya ya uongozi na kuahidi kuunga mkono shughuli za chama nchi nzima.
GAVANA NATEMBEYA NA EUGENE WAMALWA
Image: MATHEWS NDANYI
GAVANA NATEMBEYA NA EUGENE WAMALWA
Image: MATHEWS NDANYI

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ametajwa kuwa Naibu Kiongozi wa Chama cha Democratic Action Party (DAP-K).

Uamuzi huo ulipitishwa kwa kauli moja na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) katika kikao kilichofanyika kwenye hoteli ya Westside.

Mabadiliko haya ya uongozi wa chama yalipelekea pia uteuzi wa Bernard Masanja kuwa Katibu Mkuu mpya wa chama Taifa.

Masanja alijiuzulu nafasi yake ya awali ya Uongozi wa Pili wa Chama Kitaifa.

Chama kilimtaja Dick Oyugi Maungu kama Katibu Mwenezi na Mohammed Adkikarim anachukua wadhifa wa Katibu wa Uratibu wa Kaunti.

Chama hicho kinaongozwa na  Eugene Wamalwa na Natembeya aliyewania kiti cha ugavana Trans Nzoia kupitia chama hicho.

"Ninajivunia chama hiki na nina furaha kuhudumu kama Naibu kiongozi wa Chama", alisema Natembeya.

Maafisa wa chama hicho walisema uidhinishaji wa Gavana Natembya unawakilisha msukumo mkubwa kwa chama hicho, ambacho kimekuwa kikipata mafanikio kote nchini.

Uteuzi wake unatarajiwa kuimarisha uwepo wa chama hicho haswa Trans Nzoia na maeneo mengine.

Taarifa kutoka kwa pary ilisema Natembeya analeta uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma, akiwa amewahi kushika nyadhifa mbalimbali maarufu siku za nyuma.

Aliyekuwa mbunge Wafula Wamunyinyi alimkaribisha Gavana Natembeya kwa uongozi mkuu wa chama.

"Gavana ana mchango mkubwa sana katika ukuaji wa chama. Pia analeta maarifa mengi ya jinsi ya kusimamia masuala ya kaunti, ujuzi ambao unaweza kuwa na manufaa makubwa kwa chama." Alisema Wamunyinyi.

Wamalwa alisisitiza umuhimu wa kimkakati wa kujumuishwa kwa Natembeya katika uongozi wa chama, haswa katika maandalizi ya uchaguzi wa 2027.

Alionyesha imani na timu mpya ya uongozi na kuahidi kuunga mkono shughuli za chama nchi nzima.

Natembeya alisema amekubali nafasi hiyo kikamilifu na kuahidi kuhakikisha wagombea wanaostahili wanapata fursa ya kukiwakilisha chama katika uchaguzi mkuu ujao.

Gavana huyo anaungwa mkono na watu wengi huko Trans Nzoia na kuinuliwa kwake kunaweza kuimarisha taswira ya chama katika eneo hilo.