Waandamanaji wanaopinga LGBTQ watoa wito wa kufutwa kazi kwa majaji wa Kenya

Mnamo Septemba 13, 2023, Mahakama ya Upeo iliruhusu makundi ya ushoga yasijiliwe kupitia tume yao.

Muhtasari
  • Baadhi ya waandamanaji walibeba mabango ya kuwataka majaji wa Mahakama ya Juu kujiuzulu.

Maandamano dhidi ya wapenzi wa jinsia moja yalifanyika nje ya Mahakama ya Juu katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Mashirika kadhaa ya kiraia na makundi ya kidini yanaelezea kukasirishwa na uamuzi wa hivi majuzi ambao unaruhusu mashirika ya LGBTQ kujiandikisha nchini.

Baadhi ya waandamanaji walibeba mabango ya kuwataka majaji wa Mahakama ya Juu kujiuzulu.

Miaka kumi iliyopita shirika lililofadhiliwa na serikali lilikataa kusajili shirika la kutetea haki za LGBTQ likisema kwamba shirika hilo linaendeleza tabia ya watu wa mapenzi ya jinsia moja katika nchi ambayo mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo majaji mwaka huu walibatilisha uamuzi huo.

Rais wa Kenya William Ruto amewataka viongozi wa kidini kuendeleza kile anachotaja kuwa maadili ya kitamaduni.

Mnamo Septemba 13, 2023, Mahakama ya Upeo iliruhusu makundi ya ushoga yasijiliwe kupitia tume yao.

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu na majaji Smokin Wanjala na Njoki Ndung’u walisema kuwa ilikuwa kinyume cha katiba na kuwanyima haki makundi hayo haki iwapo hayangesajiliwa.

Nao majaji William Ouko na Mohamed Ibrahim walipinga wakisema hawawezi kuvumilia au kupigania haki ya watu ambao wanashiriki tabia isiyokuwa na maadili.

Maandamano ya Ijumaa yalianza katika msikiti wa Jamia hadi nje ya Mahakama ya Upeo na pia Bunge ambapo waliwasilisha malalamishi yao.

Wakitoa kauli “La ilaha illAllah Muhammadur Rasulullah’ na ‘Takbir Allah Akbar’, waumini hao walisema hawataki ushoga nchini.