"Hakuna minisketi,tumbo-cut, ku'sag!" Chuo Kikuu cha Masinde Muliro chatoa sheria kali kwa wanafunzi

Mavazi yaliyopigwa marufuku ni pamoja na sketi ndogo, suruali za kubana, tshirt za kukata tumboni na nguo za uwazi.

Muhtasari

•Uongozi wa shule hiyo ulisema kuwa umebaini kwa wasiwasi kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wakivalia isivyofaa.

•Mavazi yaliyopigwa marufuku ni pamoja na slippers, crocs, t-shirts zenye maandishi machafu, suruali iliyoshushwa (sag) na nguo zinazoonyesha kifua.

Wanawake wamevalia minisketi
Image: MAKTABA

Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST) kimetoa mwongozo mpya wa uvaaji kwa wanafunzi wake.

Katika barua ya ndani kwa wanafunzi wote ambayo ilitolewa tarehe 11 Oktoba, uongozi wa shule hiyo ulisema kuwa umebaini kwa wasiwasi kuwa baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wakivalia isivyofaa.

“Nachukua fursa hii kuwashukuru wanafunzi wote wanaovaa kwa heshima wanapofika katika chuo kikuu. Hata hivyo, tumegundua na kutambua kwa wasiwasi uvaaji usio na adabu wa baadhi yenu,” Mkuu wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Masinde Muliro, Dkt. Bernadatte Abwao alisema kwenye risala hiyo.

Mkuu huyo wa wanafunzi alibainisha kuwa wanafunzi wote, wa kiume na wa kike, wanatarajiwa kuvaa vyema wakiwa shuleni.

Kufuatia hayo, aliwaonya wanafunzi dhidi ya kuvaa baadhi ya nguo zisizo rasmi zikiwemo sketi ndogo, suruali za kubana, tshirt za kukata tumboni na nguo za uwazi.

“Zifuatazo si rasmi; Sketi ndogo/ndogo kiasi, suruali ya kubana ngozi, jeans iliyochanika, blauzi/T-shirt zilizokatwa tumboni, blauzi/nguo za chinichini, kaptura ndogo na nguo za uwazi zinazoonyesha mikanda ya sidiria,” risala hiyo ilisema. .

Mavazi mengine ambayo yalipigwa marufuku ni pamoja na slippers, crocs, t-shirts zenye maandishi machafu, suruali iliyoshushwa (sag) na nguo zinazoonyesha kifua.

"Tafadhali kumbuka kuwa slippers, crocs na viatu vyote vya plastiki sio kuvaa rasmi, na haipaswi kuvaliwa katika Chuo Kikuu. Kwa hivyo hii ni kuwaomba wanafunzi wote wavae kwa heshima,” risala hiyo ilisomeka.

Memo hiyo iliyofika Radio Jambo ilitiwa saini na mkuu wa wanafunzi Dk Benadatte Abwao kwa niaba ya Naibu Chansela na uongozi wa shule.