RIP! Radio Africa yamuomboleza mtangazaji tajika Aleem Manji

Aleem Amin Abdul Manji alifariki Novemba 12 akiwa na umri wa miaka 45.

Muhtasari

•Meneja wa wafanyikazi wa Radio Africa, Jemima Ngode alisema urithi wa kitaaluma wa Manji na maono yake yataendelezwa.

•"Nimehuzunishwa na kushtuka. Tulizungumza nawe wiki iliyopita kwenye maegesho ya gari na ulinitakia wikendi njema. Pumzika kwa amani," Ghost aliomboleza.

Marehemu Aleem Manji
Image: RADIO AFRICA

Kampuni ya Radio Africa Group, inayomiliki Radio Jambo na vituo vingine vya habari imemuomboleza marehemu Aleem Manji kama mtangazaji mahiri wa redio na kumtambua kwa  mchango wake usiofutika.

Meneja wa wafanyikazi wa Radio Africa, Jemima Ngode alisema urithi wa kitaaluma wa Manji na maono yake yataendelezwa.

"Tunapomuomboleza Aleem Manji leo, tukumbuke urithi wake wa kitaaluma, michango yake isiyofutika, upendo wake usio na kifani. Na tuendeleze maono yake, ari yake, na harakati zake za kutafuta ubora. Kwani hiyo ndiyo sifa bora kabisa tunaweza kumpa kwaheri inayofaa zaidi kwa mwenzetu marehemu," alisema.

Mtangazaji Ghost Mulee wa Radio Jambo alisema: "Nimehuzunishwa na kushtuka. Tulizungumza nawe wiki iliyopita kwenye maegesho ya gari na ulinitakia wikendi njema. Pumzika kwa amani, nafsi yenye heshima. Hakika maisha ni mafupi!"

Aleem Amin Abdul Manji alifariki Novemba 12 akiwa na umri wa miaka 45.

Mazishi ya mtangazaji huyo aliyekuwa akifanya kazi katika East FM yatafanyika Jumanne, Novemba 14 mwendo wa saa tatu na robo asubuhi katika Ukumbi wa Aga Khan Complex and Complex.

Huku wakiwa wamekaa kwenye ndoa na Bi Seema Sarkar Manji kwa miaka 13, wanandoa hao wamejaliwa watoto wawili.

"Ni kwa moyo mzito na huzuni kubwa kwamba tunatangaza kifo cha ghafla cha mtangazaji wetu Aleem Manji. Tutakukumbuka Aleem. Zaidi ya miaka 15 ya vicheko, joto, na furaha kubwa," East FM ilisema katika taarifa yake.

Waliongeza, "Mbingu imepata Malaika. Umekuwa rafiki wa ajabu, kaka, na mfanyikazi mwenza katika East FM. Roho yako ipumzike kwa amani ya milele. Tuiweke familia yake, marafiki na wafanyakazi wenzake katika mawazo na maombi yetu."