Kizaazaa kanisani mwanamke akishambuliwa kwa kisu na Ex wake wakati wa ibada

Mwathiriwa anasema alikata uhusiano na mshukiwa miezi kadhaa iliyopita baada ya kumtupa nje ya nyumba yake na hata ameolewa kwingine

Muhtasari

• Mumewe wa sasa Joshua Otieno anasema shambulio hilo lilitokea alipokuwa ametoka tu kanisani muda mfupi.

• Otieno alikimbia hadi eneo la shambulizi ili kumtazama mkewe lakini akashauriwa ajizuie.

Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Mwanamke mjamzito apatikana amedungwa visu mgongoni
Image: Maktaba//The Star

Kizaazaa kilishuhudiwa kanisani wakati wa ibada katika kaunti ya Migori baada ya mwanamke mmoja muumini kushambuliwa kwa kuchomwa kisu na mwanamume aliyetajwa kuwa ni mpenzi wake wa zamani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Citizen, Risper Akoth ambaye amelazwa hospitalini kutokana na majeraha mabaya ya kuchomwa visu, alikuwa amekwenda katika ibada ya kanisa Jumamosi iliyopita wakati mpenzi wake wa zamani alimvizia kwa kumfuata hadi kanisani na kuanza kumshambulia.

Mrembo huyo alihadithia kwamba waliachana na mume huyo miezi kadhaa iliyopita na aliingia kanisani na kumkuta ameketi kwa mahubiri kabla ya kumshambulia.

Akisimulia mkasa huo, Akoth alisema kwamba jamaa huyo baadae alitoroka kabla ya kumtishia kwamba angemuua huku waumini wengine wakiangalia tu  bila kufanya chochote.

Mwathiriwa anasema alikata uhusiano na mshukiwa miezi kadhaa iliyopita baada ya kumtupa nje ya nyumba yake na hata ameolewa kwingine, Citizen walibaini.

Mumewe wa sasa Joshua Otieno anasema shambulio hilo lilitokea alipokuwa ametoka tu kanisani muda mfupi. Otieno alikimbia hadi eneo la shambulizi ili kumtazama mkewe lakini akashauriwa ajizuie.

Wakati huo huo, babake mwathiriwa, Julius Nyambia, ametaka uchunguzi uharakishwe na kukamatwa kwa mshukiwa kwani wangetaka kujua kiini cha shambulio hilo.