Rais Ruto aidhinisha mapendekezo ya kamati ya mazungumzo ya kitaifa

Rais Ruto alipendekeza sio tu kupunguzwa kwa 30% lakini 50% ya matumizi ya serikali, akiwahimiza viongozi kuishi kulingana na uwezo wao kwa maendeleo ya Kenya.

Muhtasari

• Aidha Mkuu huyo wa Nchi aliwataka Wabunge kujadili mara moja mapendekezo ya kamati hiyo, akisisitiza uwajibikaji wa pamoja wa kuipeleka Kenya mbele.

Rais Ruto.
Rais Ruto.
Image: Facebook//WILLIAM SAMOEI RUTO

Rais William Ruto alisema kuwa amekumbatia mapendekezo kutoka kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO), iliyowasilishwa na chama tawala cha Kenya Kwanza na mungano ya upinzani Azimio la Umoja.

"Mmesikia kwamba wanaosimamia Mazungumzo wamemaliza kazi hiyo, na tunawapongeza kwa kumaliza kazi hiyo, sasa tushikane mikono na kuipeleka Kenya mbele," Ruto alisema Jumapili.

Akiwahutubia waumini wa Ushirika wa Ukuhani huko Kahawa Magharibi, Eneo Bunge la Roysambu Jumapili, Rais Ruto alipendekeza sio tu kupunguzwa kwa 30% lakini 50% ya matumizi ya serikali, akiwahimiza viongozi kuishi kulingana na uwezo wao kwa maendeleo ya Kenya.

“Wametoa mapendekezo hayo mapendekezo yote ni sawa. Ambapo walisema tunapunguza matumizi ya Serikali kwa 50%, nimeshafanya hivyo. Wanaotaka kupunguzwa kufanyike kwa 30%, nashauri waongeze hadi 50% ili Kenya isonge mbele. Ni lazima tujifunze kuishi kulingana na uwezo wetu,” aliongeza.

Aidha Mkuu huyo wa Nchi aliwataka Wabunge kujadili mara moja mapendekezo ya kamati hiyo, akisisitiza uwajibikaji wa pamoja wa kuipeleka Kenya mbele.

"Mambo mengine yote ambayo wamependekeza, sasa ni juu yenu wabunge kujadili suala hilo na kumalizana nalo ili kuendelea kufanya kazi pamoja bila chuki na migawanyiko," alisema Ruto.

Akipongeza juhudi za miezi 4 za kamati hiyo, Rais Ruto alisisitiza utendakazi wa mapendekezo yao.

Kamati hiyo, kupitia taarifa ya pamoja ya Jumamosi, Novemba 25, iliangazia haja ya kupunguza bajeti za usafiri katika mashirika ya serikali kwa asilimia 50 na kupendekeza kupunguzwa kwa Posho za Kujikimu za Kila Siku kwa Maafisa wa Serikali na Umma kwa 30%.

Hatua hiyo, kulingana na kamati hiyo, inalenga kushughulikia suala kubwa la gharama ya juu ya maisha.

Jambo lingine lililojitokeza katika mijadala ya kamati hiyo ni pendekezo la kuanzisha ofisi za Waziri Mkuu na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani.

Nafasi hizi zinazopendekezwa, zinazosubiri kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, zinaweza kushuhudia uteuzi wa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi na kinara wa upinzani Raila Odinga katika afisi husika.