KPLC yavunja kimya baada ya stima kupotea katika sehemu nyingi za Kenya, wafichua sababu

KPLC imethibitisha kurejeshwa kwa stima katika maeneo mbalimbali nchini kufuatia giza lililotanda jana usiku.

Muhtasari

•KPLC ilisema umeme umerejea katika eneo lote la Mlima Kenya, Nyanza Kusini, Magharibi, Ufa wa Kati, mikoa ya Kaskazini Mashariki na maeneo mengi ya jiji la Nairobi.

•Katika taarifa, KPLC ilisema upotevu wa umeme ulichangiwa na hitilafu inayoshukiwa kuathiri mfumo wa umeme.

Image: MAKTABA

Kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imethibitisha kurejeshwa kwa stima katika maeneo mbalimbali nchini kufuatia giza lililotanda jana usiku.

Katika sasisho la hivi punde zaidi kupitia majukwaa yake ya mitandao wa kijamii,  kampuni hiyo ilisema kuwa umeme umerejea katika eneo lote la Mlima Kenya, Nyanza Kusini, Magharibi, Ufa wa Kati, mikoa ya Kaskazini Mashariki na maeneo mengi ya jiji la Nairobi.

Pia walithibitisha kuwa walikuwa wakifanyia kazi kurejesha umeme katika eneo la Pwani na sehemu za Kaunti ya Nairobi kufikia saa nane usiku wa kuamkia Jumatatu.

"Tunawashukuru wateja wetu kwa subira yao na tunawahakikishia kuwa tunafanya kazi usiku kucha kurejesha hali ya kawaida katika maeneo yaliyosalia haraka iwezekanavyo," KPLC ilisema.

Mnamo saa tano kasoro dakika kumi  usiku wa Jumapili, kampuni hiyo ilikuwa imeripoti kwamba walikuwa wakifanya kazi ya kurejesha usambazaji wa umeme kufuatia kukatika kwa umeme kulitokea kote nchini mwendo wa saa moja jioni.

"Tunajitahidi kurejesha hali ya kawaida ndani ya muda mfupi iwezekanavyo. Taarifa kuhusu maendeleo ya urejeshaji itatolewa kwa wakati ufaao,” walisema.

"Tunaomba radhi kwa wateja wetu kwa usumbufu uliojitokeza."

Siku ya Jumapili usiku, sehemu kubwa ya nchi iliachwa katika giza totoro na kiasi baada ya umeme kupotea muda mfupi tu baada ya usiku kuingia.

Katika taarifa, KPLC ilisema upotevu wa umeme ulichangiwa na hitilafu inayoshukiwa kuathiri mfumo wa umeme.

"Tumepoteza usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na hitilafu inayoshukiwa kuathiri mfumo wa umeme," KPLC ilisema kwenye taarifa.

Kampuni hiyo ilikuwa imewataka Wakenya kuwa watulivu wanaposhughulikia kurejesha mamlaka ndani ya muda mfupi.