Nyeri: Makumi ya vijana wakamatwa na polisi kwa kuhusishwa na kundi haramu la Mungiki

Katika msako huo, makumi ya vijana walitiwa mbaroni na kupakizwa katika magari ya polisi mithili ya shehena ya magunia ya maharagwe.

Muhtasari

• Katika msako huo, makumi ya vijana walitiwa mbaroni na kupakizwa katika magari ya polisi mithili ya shehena ya magunia ya maharagwe.

• Kwa mujibu wa kamishna wa polisi wa Nyeri Pius Murugu, mkutano wa Maina Njenga ulikuwa haramu na haukuwa na kibali cha kuandaliwa kwa namna yoyote ile.

Nyeri polisi waliwakamata waliohusishwa na Mungiki
Nyeri polisi waliwakamata waliohusishwa na Mungiki
Image: Hisani

Wikenedi iliyopita makumi ya vijana mjini Nyeri walitiwa mbaroni na polisi katika msako ulionuia kuzima mkutano uliotarajiwa kufanyika mjini humo na kuongozwa na aliyekuwa kiongozi wa kundi haramu la Mungiki, Maina Njenga.

Kwa mujibu wa picha na video zilizoenezwa katika mitandao ya kijamii Jumapili ya mwisho ya mwaka 2023, polisi waliweka vizuizi katika barabara mbalimbali za kuingia mjini Nyeri na kufanya msako mkali katika kila gari lililokuwa likiingia humo.

Msako huu ulinuiwa kuwakamata watu ambao walikuwa wanaelekea kuhudhuria katika mkutano huo ambao vyombo vya dola vilihisi ni wa kulifufua kundi hilo haramu lililotokomezwa takribani miongo miwili iliyopita.

Katika msako huo, makumi ya vijana walitiwa mbaroni na kupakizwa katika magari ya polisi mithili ya shehena ya magunia ya maharagwe.

Kwa mujibu wa kamishna wa polisi wa Nyeri Pius Murugu, mkutano wa Maina Njenga ulikuwa haramu na haukuwa na kibali cha kuandaliwa kwa namna yoyote ile.

“Tuna maelezo kwamba kuna baadhi ya watu wanataka kufanya mkutano huku na kusambaratisha Amani, hatutakubali mkutano wa aina hiyo katika eneo letu. Kaunti ya Nyeri imekuwa ya Amani na hatutatoa nafasi yoyote ya kuwaweka wananchi wetu katika tisho la ukosefu wa Amani na usalama,” Murugu alinukuliwa na gazeti la Nation.