Mvulana miaka 11 miongoni mwa watu 23 waliokamatwa Murang'a wakituhumiwa kuwa Mungiki

Miongoni mwa vitu vilivyopatikana katika kundi hilo ni tumbaku, pembe, miwa, pombe ya kitamaduni ya muratina, whisky, na bendera yenye rangi tatu ambazo kwa kawaida huhusishwa na kundi hilo lenye itikadi kali.

Muhtasari

• Wameanzisha uchunguzi wakidai kuwa watu hao wanaweza kuwa na uhusiano na kundi lililoharamishwa la Mungiki.

• "Tulipata habari kuwa kulikuwa na watu kwenye hekalu hilo na shughuli zao zilitiliwa shaka na wenyeji," Kainga alisema kama alivyonukuliwa na K24.

Nyeri polisi waliwakamata waliohusishwa na Mungiki
Nyeri polisi waliwakamata waliohusishwa na Mungiki
Image: Hisani

Jumapili ya Desemba 31 mwaka jana, msako dhidi ya kundi haramu la Mungiki ulifanyika katika maeneo mbali mbali ukanda wa Mlima Kenya, baada ya vyombo vya dola kupata ripoti kwamba Maina Njenga alikuwa ameratibu mkutano wake katika kaunti ya Nyeri.

Taarifa kutoka kaunti ya Murang’a zinadai kwamba watu 23 walitiwa nguvuni na polisi wakituhumiwa kuwa wanajihusisha na itikadi kali za kundi hilo lililoharamishwa takribani miongo miwili iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti ya K24, kati ya 23 hao ni wanawake 11, wanaume 11 na mtoto mmoja mvulana anayekadiriwa kuwa wa umri wa miaka 11.

Watu hao walikamatwa katika eneo la Mukurwe wa Nyagathanga wakiwa na vitu ambavyo vinakisiwa kuwa na ishara zote kuwa huenda wakawa wale wanaojihusisha na kundi hilo haramu.

K24 waliripoti kwamba Polisi, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi, waliwavizia watu hao walipokuwa wakichinja mbuzi kwenye hekalu linaloaminika kuwa chimbuko la jamii ya Wakikuyu.

Kamanda wa polisi wa Kaunti ya Murang'a David Kainga alisema kuwa walitahadharishwa kuhusu shughuli za kutiliwa shaka katika hekalu hilo na wakaazi wanaoishi karibu na eneo hilo.

Alitaja 10 kati ya waliokamatwa wanatoka Nairobi, huku wengine 13 wakiwa wenyeji. Wameanzisha uchunguzi wakidai kuwa watu hao wanaweza kuwa na uhusiano na kundi lililoharamishwa la Mungiki.

"Tulipata habari kuwa kulikuwa na watu kwenye hekalu hilo na shughuli zao zilitiliwa shaka na wenyeji," Kainga alisema kama alivyonukuliwa na K24.

Miongoni mwa vitu vilivyopatikana katika kundi hilo ni tumbaku, pembe, miwa, pombe ya kitamaduni ya muratina, whisky, na bendera yenye rangi tatu ambazo kwa kawaida huhusishwa na kundi hilo lenye itikadi kali.

Kundi hilo, hata hivyo, lilikanusha madai ya kuwa na uhusiano na dhehebu la Mungiki, likisema kuwa walikuwa wamekwenda huko kujifunza zaidi kuhusu mila za kitamaduni.