Polisi walisambaratisha sherehe za birthday ya Raila kuchukuliwa hatua - IG Koome

Wafuasi wa Odinga waliojumuika Nairobi CBD kwa ajili ya kukata keki walitawanywa na polisi kwa kutupiwa vitoa machozi, kitendo ambacho IG amelaani vikali.

Muhtasari

• Kupitia taarifa iliyotolewa jioni, Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ilitaja hatua za maafisa hao kuwa kinyume cha sheria.

• "Huduma ya Kitaifa ya Polisi inasisitiza dhamira yake ya kutoegemea upande wowote wa kisiasa katika kutekeleza jukumu lake la kulinda maisha na mali."

vitoa machozi
vitoa machozi
Image: Screengrab

Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome amelaani vikali kitendo cha maafisa wa polisi kusambaratisha mkutano wa wafuasi wa kinara wa upinzani Raila Odinga ambao walijumuika kusherehekea siku ya kuzaliwa ya kiongozi huyo.

Jumapili, Odinga alikuwa akiadhimisha miaka 79 na mamia ya wafuasi wake kutoka pande mbalimbali walifurika mitandaoni wakimtakia heri njema, huku wengine wakikwenda hatua Zaidi kuandaa mkutano wa kuvunja keki kumsherehekea.

Waliojumuika katikati wa jiji la Nairobi katika mkutano wa Amani wakimuimbia nyimbo za kumsifu na kumtakia heri njema Odinga walivurugwa na polisi kwa kutawanywa na vitoza machozi.

Kupitia taarifa iliyotolewa jioni, Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ilitaja hatua za maafisa hao kuwa kinyume cha sheria.

“Huduma ya Kitaifa ya Polisi inatambua mtawanyiko wa ghasia usio na msingi wa wananchi waliokuwa wakifanya sherehe za amani jijini Nairobi leo 7/7/2024. Inspekta Jenerali, IG Japhet Koome ameagiza hatua kali za kiutawala zichukuliwe dhidi ya Maafisa waliohusika na kitendo hicho kinyume cha sheria,” ilisema.

"Huduma ya Kitaifa ya Polisi inasisitiza dhamira yake ya kutoegemea upande wowote wa kisiasa katika kutekeleza jukumu lake la kulinda maisha na mali."

Odinga, ambaye anaongoza muungano wa Azimio La Umoja One Kenya, mwenyewe aliripotiwa kutokuwepo wakati wa kisa hicho, huku kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka akisema alikuwa mbali huko Malindi, Kaunti ya Kilifi.