"Alikuwa na kisu!" Salasya avunja kimya kuhusu tukio ambapo alimpiga MCA kofi moto

Mbunge huyo alidai kuwa MCA ambaye alipiga kofi alikuwa akimchokoza huku akiwa amejihami kwa kisu.

Muhtasari

•Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alimshutumu gavana wa Kakamega Fernandes Barasa kwa kuwalipa MCAs ili kumshambulia.

•Mbunge huyo alidai kuwa MCA ambaye alipiga kofi Ijumaa alikuwa akimtishia wakati alipokuwa akitoa hotuba yake.

alimpiga kofi mwombolezaji siku ya Ijumaa.
Mbunge Peter Salasya alimpiga kofi mwombolezaji siku ya Ijumaa.
Image: HISANI

Mbunge wa Mumia Mashariki Peter Salasya amejitokeza kujitetea baada ya drama iliyomhusisha kuibuka katika hafla ya mazishi aliyokuwa amehudhuria Ijumaa wiki jana.

Wiki jana, mwanasiasa huyo aliyezingirwa na drama alikamatwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana ya Ksh50,000 pesa taslimu baada ya kumvamia mwakilishi wa wadi wakati wa mazishi ya Jesmus Kodia katika kijiji cha Maraba kaunti ya Kakamega.

Wakati akijitetea Jumapili, mbunge huyo wa muhula wa kwanza alimshutumu gavana wa Kakamega Fernandes Barasa kwa kuwalipa MCAs ili kumshambulia.

“Wananitusi, wanapiga gari wanapasua ili nisiongee chochote. Ni wahuni wangapi ambao wamenishambulia hadharani na sijawagusa?,” Salasya alilalamika kwenye taarifa ya video.

Mbunge huyo wa DAP-K alidai kuwa MCA alimwendea akiwa ameketi kwa utulivu na kuanza kumuonya dhidi ya kumzungumzia yeye au gavana.

Pia alidai kuwa MCA ambaye alipiga kofi Ijumaa alikuwa akimtishia wakati alipokuwa akitoa hotuba yake katika hafla ya mazishi waliyokuwa wamehudhuria.

“Alikuwa akinichokoza. Na wakenya wananitusi. Msinitusi bila kuuliza tatizo liko wapi. Mimi ni mtu wa amani sana, isipokuwa mtu atanichokoza,” alisema.

Aliongeza, “Sasa kama huyo MCA alikuwa hapo alikuwa amejihami na kisu chake pale. Sasa mimi nikiongea walinipata offguard, sasa ningefanya aje? Ningefanya namna gani? Ati nisionee."

Salasya aliwataka wanamitandao kuwa wenye kuelewa katika uamuzi wao na kutafuta kujua tatizo ni nini kabla ya kuendelea kumtukana.

Huku haya yakijiri, Chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) kimemwita mbunge huyo wa Mumias kwa mkutano siku ya Jumanne.

Akifichua maelezo wakati wa mazungumzo katika kituo kimoja cha redio cha humu nchini, kiongozi wa chama cha DAP K Eugene Wamalwa Jumatatu alisema kuwa uongozi wa chama hicho utakutana na mbunge huyo baada ya kufika mahakamani.

“Tumemuita (Salaysa) na anafikishwa mahakamani kesho na baada ya hapo atakuja kukutana na uongozi wa chama,” alisema.

Wamalwa alimtaja mbunge huyo wa muhula wa kwanza kama kijana maarufu sana ambaye huenda anahusika na masuala ya kudhibiti hasira.

Licha ya hayo, waziri huyo wa zamani wa Ulinzi anaangazia kuwa chama bado kitamshauri Salasya.

"Yeye( Salaysa) ni kiongozi asiye na woga ambaye alipigania Mumias Sugar na watu wake. Lakini anahitaji kusimamia baadhi ya masuala anayolaumiwa," Wamalwa aliongeza.