Mwanafunzi wa kidato cha kwanza afariki kwa kutatanisha siku kumi baada ya kudahiliwa

Kwa mujibu wa Lisa Mwongera, shangazi wa marehemu, mwili huo ulikuwa na michubuko kwenye paji la uso, jambo ambalo haliendani na nadharia ya kuugua tumbo.

Muhtasari

• Familia hiyo inaamini huenda mwanafunzi huyo alidhulumiwa kupita kiasi na kwamba shule haikuwa ikifichua kikamilifu kilichotokea.

Picha ya maktaba ya gari la Polisi la Kitengela katika eneo la uhalifu hapo awali.
Image: MAKTABA

Familia ya mwanafunzi wa kidato cha kwanza aliyefariki katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kilungu kaunti ya Makueni mnamo Alhamisi wiki jana inalilia haki baada ya shule hiyo kutoa maelezo yanayokinzana.

Kwa mujibu wa NTV Kenya, Emmanuel Kirimi Kaimenyi, ambaye alikuwa amedahiliwa katika shule hiyo siku kumi tu zilizopita anasemekana aliugua asubuhi ya Alhamisi, Januari 25 na kukimbizwa katika Hospitali Ndogo ya Kaunti ya Kilungu, ambapo alithibitishwa kufariki alipofika.

Mkuu wa shule hiyo Geoffrey Muema alisema mtoto huyo alilalamikia maumivu ya tumbo na kupelekwa katika kituo cha afya cha serikali kilichopo umbali wa mita 800 kutoka shuleni hapo.

“Mwanafunzi huyo alimwomba mwanafunzi mwenzake mmoja amsindikize vyooni na hali yake ikawa mbaya ghafla. Alipoteza fahamu na kukimbizwa katika hospitali ya jirani na walimu wawili,” alisema mkuu wa shule kwa mujibu wa NTV.

Kimeu anasema aliitwa na walimu muda mfupi baadaye na kutakiwa kuungana nao baada ya madaktari katika hospitali hiyo kushindwa kumfufua kijana huyo.

Mkuu wa shule anasema mvulana huyo aliugua dakika kadhaa hadi saa kumi na akapoteza fahamu haraka na akafa saa tano asubuhi.

"Mara moja niliita afisi ya Elimu na kuwapa maelezo kisha nikaendelea kuripoti kifo cha ghafla cha mwanafunzi huyo katika kituo cha polisi cha Kilungu," aliambia Sunday Nation.

Ni baada ya hayo ambapo Muema aliwapigia simu wazazi wa mwanafunzi huyo akimtaka babake Joshua Kaimenyi afike katika shule ambayo mwanawe alikuwa akiugua.

Baba huyo alisafiri kutoka Isinya katika Kaunti ya Kajiado na kufika Kilungu mwendo wa saa kumi na mbili jioni ambapo habari hiyo ya kusikitisha ilimfikia. Kufikia wakati huu, mwili wa mwanafunzi huyo ulikuwa tayari umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Kilungu.

Familia hiyo inaamini huenda mwanafunzi huyo alidhulumiwa kupita kiasi na kwamba shule haikuwa ikifichua kikamilifu kilichotokea.

Kwa mujibu wa Lisa Mwongera, shangazi wa marehemu, mwili huo ulikuwa na michubuko kwenye paji la uso, jambo ambalo haliendani na nadharia ya kuugua tumbo.

Mwongera ambaye alizungumza kwa niaba ya familia alisema wamebaini kuwa mtoto huyo alipelekwa katika kituo cha afya cha binafsi kilichopo kati ya shule hiyo na Hospitali ya Kata ya Kilungu, ambapo alifikwa na umauti.

"Wakati wote huo mkuu wa shule hakuwahi kutueleza ukweli huo, lakini hospitali hiyo ya kibinafsi - Winesa Medical Center ilituthibitishia kwamba walipokea mwili wa mwanafunzi kutoka shule hiyo saa 10:40 asubuhi" alisema Mwongera.