DCI yachapisha majina, utambulisho wa washukiwa katika mlipuko wa gesi Embakasi uliwaua 6

Waathiriwa 6 wamefariki huku watu wengine wapatao 300 wakiripotiwa kuwa na viwango tofauti vya majeraha ya moto.

Muhtasari

•DCI imefichua kuwa kufikia sasa, watu wanne wamekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.

•Mmiliki wa eneo hilo haramu la kujaza gesi, Derrick Kimathi ni miongoni mwa wale ambao wamekamatwa.

ni miongoni mwa wanaotafutwa na DCI
Robert Gitau, Ann Kaburi na Joseph Makau ni miongoni mwa wanaotafutwa na DCI
Image: DCI//

Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) inaendelea na uchunguzi kuhusu kisa cha mlipuko hatari wa gesi uliotokea katika mtaa wa Embakasi, Nairobi mnamo Februari 1, 2024, na kuua watu watatu papo hapo na kuwaacha wengine wengi na majeraha tofauti.

Katika ripoti ya Jumanne asubuhi, Februari 6, wapelelezi walifichua kuwa kufikia sasa, watu wanne wamekamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi kuhusiana na tukio hilo la kusikitisha.

Mfanyibiashara anayeaminika kuwa mmiliki wa eneo hilo haramu la kujaza gesi, Derrick Kimathi ni miongoni mwa wale ambao wamekamatwa. Maafisa watatu wa NEMA pia wako kizuizini.

"DCI inaendelea kuzipa pole familia za waliopoteza maisha yao, na inawatakia ahueni ya haraka wale wanaopata nafuu katika vituo mbalimbali vya afya," DCI ilisema katika taarifa Jumanne asubuhi.

Taarifa hiyo ilisomeka zaidi, "Wakati huo huo, ili kuhakikisha kuwa haki imetendeka, timu za DCI zinazochunguza tukio hilo baya hadi sasa zimemkamata mshukiwa mkuu Derrick Kimathi pamoja na maafisa watatu wa NEMA ambao walipatikana na hatia."

Maafisa wa NEMA ambao wako chini ya ulinzi wa polisi ni pamoja na mkurugenzi wa uzingatiaji mazingira David Ongare, mkuu wa tathmini ya athari za mazingira Joseph Makau na afisa mwingine aliyetambuliwa kama Mirrian Kioko.

Idara ya DCI inaendelea na msako wa washukiwa wengine watano waliohusishwa na tukio hilo la mapema Februari ambao wanaripotiwa kuwa mafichoni. Wao ni pamoja na; Stephen Kilonzo (msimamizi wa tovuti), Ann Kabiri Mirungi wa NEMA, Lynette Cheruyoit (Afisa Mwandamizi wa Mazingira wa NEMA), dereva wa lori Robert Gitau na Abraham Mwangi (dereva).

"Iwapo utakuwa na taarifa kuhusu mshukiwa yeyote aliko, tafadhali #FichuakwaDCI kwa kupiga simu yetu ya bure 0800722203 au uripoti katika kituo chochote cha polisi," DCI ilisema.

Kufikia sasa, waathiriwa sita wa mlipuko huo mbaya wa gesi wamefariki huku watu wengine wapatao mia tatu wakiripotiwa kujeruhiwa kwa viwango tofauti vya moto.

Baadhi ya waathiriwa walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani huku wengine wakiwa bado wamelazwa katika hospitali mbalimbali wakiwa katika hali tofauti.