Wakenya wafanyakazi wanapokea mishahara ya chini kulinganishwa na ya kabla ya Covid-19

Ripoti hiyo ilibaini kwamba Wakenya wengi sasa wamekimbilia kuchukua mikopo ili kutatua matatizo yao ya kifedha.

Muhtasari

• Utafiti uliokusudia kubaini tabia ya Wakenya katika matumizi ya pesa na jinsi wanavyojimudu katika mazingira mbalimbali ya uchumi unaobadilika.

PESA ZA KENYA
PESA ZA KENYA
Image: STAR

Asilimia 62 ya Wakenya walioajiriwa katika sekta mbalimbali sasa imebainika kwamba wanapokea kima cha chini cha mishahara ikilinganishwa na kiwango ambacho walikuwa wanapokea kabla ya ujio wa janga la Covid-19.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopeperushwa na runinga ya NTV Kenya, asilimia 10 pekee ya Wakenya ndio imekiri kupata nyongeza ya mishahara ikilinganishwa na ile waliyokuwa wakilpwa kabla ya Covid-19.

Ripoti hiyo ilisema kwamba idadi kubwa ya walioathirika na ushuru huo mkubwa unaokata mishahara pakubwa ni wanawake ambao wanapata mishahara ya chini kwa asilimia 65 ikilinganishwa na asilimia 59 ya wenzao wa kiume.

Utafiti huo ulifanikishwa na Old Mutual Financial Services Monitor, utafiti uliokusudia kubaini tabia ya Wakenya katika matumizi ya pesa na jinsi wanavyojimudu katika mazingira mbalimbali ya uchumi unaobadilika.

Ripoti hiyo ilibaini kwamba Wakenya wengi sasa wamekimbilia kuchukua mikopo ili kutatua matatizo yao ya kifedha.

“Ufikiaji wa mikopo nchini Kenya umekuwa na uwazi mkubwa, ni moja ya bidhaa ya kifedha ambayo inakua kwa kasi Zaidi. Ujio wa mikopo kwa njia za kidijitali kupitia benki na wakopeshaji wengine katika soko utaenda kuongeza kasi hiyo hata Zaidi,” Arthur Oginga, CEO wa Old Mutual kanda ya Afrika Mashariki alisema.

“Ukweli kwamba Wakenya sasa hawahitaji kwenda kupanga foleni ndefu, kuketi kwenye benki au kusubiri kwa siku kadhaa kupata jawabu, lakini kwamba sasa wanatumia intaneti na sekunde mbili wamepata jawabu la kukataliwa au kukubaliwa mkopo, hili litachangia ufikiaji wa haraka wa huduma za mikopo,” aliongeza.