Mazungumzo ya mwisho kati ya mwanariadha Kiptum na baba yake kabla ya kuaga dunia

Akiwa amehuzunishwa na kifo cha mwanawe, ambaye ameacha watoto, Cheruiyot ametoa wito kwa serikali ya Kenya kufanya uchunguzi kuhusu kifo cha mwanariadha huyo.

Muhtasari
  • Babake Kiptum alisema alikuwa amezungumza naye mara ya mwisho Jumamosi, ambapo mwanariadha huyo alimpa hakikisho la medali zaidi na mustakabali mwema.
BABA YAKE MWANARIADHA KELVIN KIPTUM
Image: HISANI

Ulimwengu unaomboleza kifo cha kusikitisha cha mwanariadha Kelvin Kiptum, ambaye aliaga dunia kutokana na majeraha aliyopata kwenye ajali ya barabarani Jumapili, Februari 11, 2024.

Nyota anayechipukia, ambaye aliweka Kenya kwenye ramani ya dunia alipokimbia marathon kwa saa 2:00:35 mnamo Oktoba 2023, alikuwa mtoto wa pekee kwa Samson Cheruiyot.

Akiwa amehuzunishwa na kifo cha mwanawe, ambaye ameacha watoto, Cheruiyot ametoa wito kwa serikali ya Kenya kufanya uchunguzi kuhusu kifo cha mwanariadha huyo.

"Nilipata taarifa za kifo cha mwanangu nilipokuwa nikitazama habari. Nilienda eneo la ajali lakini polisi walikuwa wameupeleka mwili huo Eldoret,” Cheruiyot anakumbuka.

Babake Kiptum alisema alikuwa amezungumza naye mara ya mwisho Jumamosi, ambapo mwanariadha huyo alimpa hakikisho la medali zaidi na mustakabali mwema.

“Aliniambia mtu atakuja kutusaidia kujenga nyumba. Alisema kuwa mwili wake sasa uko sawa, na sasa anaweza kukimbia kwa 1:59,” Cheruiyot alikumbuka mazungumzo ya mwisho na mwanawe wa pekee.

“Kiptum alikuwa mtoto wangu wa pekee. Ameniacha mimi, mama yake na watoto wake. Sina mtoto mwingine. Mama yake alikuwa mgonjwa kwa muda. Sasa hivi nina huzuni kubwa.”

Huku akitaka uchunguzi ufanyike kuhusu kifo hicho, Cheruiyot alisema watu wasiojulikana walikuwa wamezuru nyumbani kwake hivi majuzi kumtafuta Kiptum.

“Kuna watu waliokuja nyumbani kitambo waliokuwa wakimtafuta Kiptum lakini walikataa kujitambulisha. Niliwauliza watoe kitambulisho, lakini waliamua kuondoka. Lilikuwa kundi la watu 4,” alisema, na kuitaka serikali kuingilia kati katika kusomesha watoto wa mbio za marathoni.