Homa Bay: Mwalimu mstaafu adaiwa kumlawiti mvulana wa miaka 7 kwa kumrubuni na Sh10

Kulingana na polisi, mvulana huyo alifichua kwa mamake kwamba mwalimu huyo mstaafu alimrubuni na kumlawiti.

Muhtasari

• Kulingana na polisi, mvulana huyo alifichua kwa mamake kwamba mwalimu huyo mstaafu alimrubuni na kumlawiti.

Kijana alawitiwa na dereva bosi wake
Kijana alawitiwa na dereva bosi wake
Image: BBC NEWS

Polisi katika eneo la Rachuonyo Kaskazini, Kaunti ya Homa Bay wanachunguza kisa ambapo mvulana wa umri wa miaka 7 alidaiwa kulawitiwa na mwalimu mstaafu wa shule ya msingi katika kijiji cha Kotolo.

Kwa mujibu wa Citizen, Mwanafunzi huyo wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya eneo hilo anasemekana kulawitiwa na mshukiwa ndani ya nyumba yake Jumanne usiku.

Kulingana na polisi, mvulana huyo alifichua kwa mamake kwamba mwalimu huyo mstaafu alimrubuni na kumlawiti.

Chifu wa Kakdhimu Magharibi Margaret Ager anasema mamake mvulana huyo aliripoti kisa hicho kwa chifu msaidizi wa lokesheni ndogo ya Kayoo kwamba mshukiwa alitenda kitendo hicho cha kinyama na kumuonya mtoto huyo kutofichua.

Ager anasema mara moja walimkimbiza mvulana huyo katika kituo cha afya cha eneo hilo ambapo ripoti ya matibabu ilithibitisha kwamba alilawitiwa.

Msimamizi huyo anasema kuwa mshukiwa alimrubuni mwathiriwa kwa Ksh.10 na kumpeleka nyumbani kwake ambapo alimdhulumu na kumuonya kutofichua kwa mtu yeyote.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Rachuonyo Kaskazini Lydia Partiyie, ambaye alithibitisha kisa hicho, anasema wanamsaka mshukiwa ambaye bado hajakamatwa baada ya kutenda kosa hilo.