Kwa nini Raila ndiye mgombea bora wa nafasi ya juu ya AU - Orengo

Alisema ODM itasalia kuwa vuguvugu la kimaendeleo na "ngome ya uhuru, haki na demokrasia na utawala wa sheria."

Muhtasari

• Gavana huyo wa Siaya aliongeza kuwa Raila amejenga mfumo wa kisiasa na msingi wa kitaifa na uungwaji mkono ambao hauwezi kusambaratika.

• Alisema ODM itasalia kuwa vuguvugu la kimaendeleo na "ngome ya uhuru, haki na demokrasia na utawala wa sheria."

ORENGO
ORENGO
Image: Hisani

Gavana wa Siaya James Orengo ameidhinisha kuteuliwa kwa kinara wa Upinzani Raila Odinga kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Mshirika wa muda mrefu wa Raila, Orengo alisema kiongozi huyo wa ODM ana tajriba kubwa, sifa zisizo na kasoro na maono mazuri kwa watu na bara la Afrika.

"Ndani yake, Afrika itakuwa na sauti yenye nguvu na itaweza kutengeneza mpango unaokubalika wa kutumia rasilimali nyingi za Afrika kwa manufaa na ustawi wa bara na mabadiliko ya watu wetu," alisema kwenye X.

Orengo aliongeza kuwa katika jukwaa la dunia, Raila ataendeleza amani miongoni mwa Mataifa, kugeuza mipaka kuwa madaraja ya fursa na kuendeleza uanachama wa kudumu wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

"Sina shaka kwamba jukumu hili jipya halitatenga ushiriki wa Raila Odinga katika masuala ya Kenya kama mzalendo na raia na haki zake zote na uhuru hazijasitishwa na hazitasitishwa," alisema.

Gavana huyo wa Siaya aliongeza kuwa Raila amejenga mfumo wa kisiasa na msingi wa kitaifa na uungwaji mkono ambao hauwezi kusambaratika.

Alisema ODM itasalia kuwa vuguvugu la kimaendeleo na "ngome ya uhuru, haki na demokrasia na utawala wa sheria."

Rais wa zamani wa Nigeria Olusegun Obasanjo pia amemuidhinisha Raila kuwania nafasi hiyo.

Obasanjo alisema hana shaka kuwa kiongozi huyo wa Upinzani ni mgombea halali wa nafasi hiyo iwapo ataungwa mkono na ukanda wa Afrika Mashariki.

"Sina shaka kwamba rafiki yangu ni mgombea anayefaa lakini chini ya maoni, hisia, misimamo na mawasilisho ya viongozi wetu katika ukanda wa Afrika Mashariki," alisema Alhamisi.

Mwenyekiti wa sasa Moussa Faki Mahamat anatazamiwa kuondoka madarakani Machi mwaka ujao.

Mwenyekiti mpya atachaguliwa katika mkutano ujao wa AU, mwaka wa 2025.