'kuna watoto wa kwanza kuangaliwa,'Gachagua aendeleza matamshi ya umiliki wa Serikali

Gachagua alizungumza katika Eneobunge la Mosop, Kaunti ya Nandi, ambako aliongoza maafisa wengine wa serikali kwenye ibada ya kanisa

Muhtasari
  • DP Gachagua pia alielezea hatua ambazo serikali inapanga kuchukua ili kukabiliana na tishio la pombe haramu nchini.
DP Gachagua
DP Gachagua
Image: Facebook

Naibu Rais Rigathi Gachagua amezungumzia tena simulizi la umiliki wa hisa za kisiasa, akisema utawala wa Kenya Kwanza utawapa kipaumbele Wakenya walioupigia kura katika usambazaji wa nafasi za ajira za serikali na miradi ya maendeleo.

Gachagua alizungumza katika Eneobunge la Mosop, Kaunti ya Nandi, ambako aliongoza maafisa wengine wa serikali kwenye ibada ya kanisa na baadaye kuchangisha pesa katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kurgung.

Alitoa wito kwa wenyeji wa Kaunti ya Nandi kusalia na subira huku Jimbo likishughulikia miradi ya maendeleo na nafasi za ajira ambazo zitawapa kipaumbele wafuasi wa Kenya Kwanza.

“Rais yuko pale, mimi niko hapo, huyu Felix ako hapo, Raisi mnamjua, mimi mnanijua msimamo wangu wa kwamba watoto wakiwa wengi, kuna wale wa kwanza wa kuangaliwa, si mnajua? Sasa huyu Felix ako hapo, na ndio mwenye kuunganisha waya, mambo yenu tumepanga,” alisema.

Matamshi yake yalikuwa sawa na mara ya mwisho alipoibua mijadala ya umma kwa kudokeza upendeleo kwa Wakenya walioipigia kura serikali.

Aliongeza: “Mambo iko sawa. Chakula iko jikoni, karibu kuiva. Watoto ni wengi, chakula ni kidogo. Iko watoto wa nyumbani, iko wa jirani, iko namna hii, namna hii, nyinyi mtulie. Chakula ikiiva, sisi ndio wenye kuleta, na watoto tunawajua kwa sura na msimamo. Hatuwezi kuchanganyikiwa, kuna mtu hajui watoto wake?”

DP Gachagua pia alielezea hatua ambazo serikali inapanga kuchukua ili kukabiliana na tishio la pombe haramu nchini.

“Na wiki inayokuja tutatangaza hatua kali tutakayo chukua, na ile maneno tumepanga, hii watu wanauza pombe haramu watahama hii nchi. Watahama hii Kenya. Tutatangaza,” alisema.