Mwili wa mwanafunzi wa chuo kikuu wapatikana shimoni Machakos

Okanda alisema mwili wa marehemu ulitolewa kwenye mtaro kando ya mtaa wa Ilovia huko Katoloni.

Muhtasari
  • Mwili wa mwanafunzi huyo ulitolewa kwenye mtaro ndani ya Kitongoji cha Machakos Alhamisi usiku.
Crime Scene
Image: HISANI

Mwanafunzi wa kike wa chuo kikuu amefariki katika hali tatanishi kaunti ya Machakos.

Mwili wa mwanafunzi huyo ulitolewa kwenye mtaro ndani ya Kitongoji cha Machakos Alhamisi usiku.

Kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Machakos Emmanuel Okanda alisema kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 11.20 jioni na kuripotiwa katika kituo cha polisi cha Machakos kama kisa cha kifo cha ghafla.

Okanda alisema mwanafunzi huyo wa mwaka wa kwanza alisemekana kuondoka katika nyumba yake ya kupanga huko Katoloni ndani ya Mji wa Machakos kwa ajili ya chakula cha jioni katika hoteli moja eneo hilo tukio lilipotokea.

"Ninathibitisha kifo cha mwanafunzi huyo, alikuwa ameenda kula chakula cha jioni na akafa," Okanda aliambia Radiojambo katika ofisi yake mjini Machakos siku ya Ijumaa.

Okanda alisema mwili wa marehemu ulitolewa kwenye mtaro kando ya mtaa wa Ilovia huko Katoloni.

Alisema haikuwa na majeraha yanayoonekana wakati ilipokusanywa na maafisa wa polisi kutoka kituoni.

"Tumeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo," Okanda alisema.

Mkuu huyo wa polisi alisema mwili huo umehamishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti katika kaunti hiyo.