•Familia ilifichua kuwa marehemu mwanahabari huyo atazikwa nyumbani kwao Noosupeni Farm Olokirikirai, kaunti ya Narok.
•Alikuwa binti wa marehemu Dominic na Mary Yiapan. Alikuwa na ndugu sita, wapwa kadhaa na wajukuu.
Marehemu mwanahabari wa NTV Rita Tinina Yiapan atazikwa Jumatano, Machi 27.
Familia, katika tangazo la kifo ilifichua kuwa marehemu mwanahabari huyo atazikwa nyumbani kwao Noosupeni Farm Olokirikirai, katika, kaunti ya Narok.
"Mwili utaondoka Umash Funeral Home Nakuru tarehe 27 Machi 2024 saa moja asubuhi kwa ibada ya mazishi na maziko itafanyika nyumbani kwao, Noosupeni Farm Olokirikirai, kaunti ya Narok kuanzia saa nne asubuhi," tangazo la kifo na mazishi lililofikia kwa Radio Jambo lilisomeka.
“Mikutano ya maandalizi ya mazishi inafanywa katika Kanisa la All-Saints Cathedral kuanzia saa kumi na moja unusu jioni. Misa ya wafu itafanyika katika Kanisa la Holy Family Basilica tarehe 25 Machi kuanzia saa nne asubuhi”
Katika tangazo la mazishi, pia ilifichuliwa kwamba mwandishi huyo wa habari alikuwa mshirika wa Robert Nagila na mama wa Mia Malaikah.
Alikuwa binti wa marehemu Dominic na Mary Yiapan. Alikuwa na ndugu sita, wapwa kadhaa na wajukuu.
"Katika wakati huu wa maombolezo, tuheshimu kumbukumbu yake kwa kumkumbuka na shukrani kwa upendo alioshiriki nasi sote," familia ilisema.
Mwanahabari Rita Tinina alipatikana akiwa amefariki Jumapili iliyopita katika nyumba yake katika mtaa wa Kileleshwa.
Uchunguzi wa maiti uliofanyika kwenye mwili wake ulibaini alifariki kutokana na nimonia kali.
Akizungumza katika mochari ya Umash Funeral Home, msemaji wa familia Timothy Njaga alisema wameridhishwa na matokeo hayo.
“Tulikuwa tumekuja hapa kushuhudia uchunguzi wa maiti na ukamilishwa na Dk Ndegwa na mwanapatholjioa wa familia. Tumepewa matokeo kuwa marehemu Rita alifariki kwa nimonia kali,” alisema.
Njaga alisema daktari wa mwanapathojia wa serikali Peter Ndegwa alifanya uchunguzi huo mbele ya mwanapathojia wa familia.
Pia alisema familia bado inaomba faragha na nafasi.
"Tunapaswa kukumbuka kuwa kuna familia ambayo imeathirika," Njaga alisema.
"Tunashukuru wanahabari kwa maneno yao mazuri kwa dada na rafiki yetu."
Baadhi ya wanahabari waliokuwepo wakati wa zoezi hilo ni pamoja na rais wa Chama cha Wahariri Kenya Zubeida Kananu na mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari wa Bunge la Kenya Duncan Khaemba miongoni mwa wengine.