Chuo kikuu cha Moi chavunja kimya baada ya basi lililokuwa na wanafunzi 65 kupata ajali

Taasisi ilifichua kuwa basi hilo lilikuwa na wanafunzi 65 waliokuwa wakienda kwa Safari ya Kimasomo..

Muhtasari

•Taasisi hiyo ambayo ina makao yake mjini Eldoret ilithibitisha kuwa ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa nne alfajiri.

•Naibu Chansela alitangaza kuwa kwa bahati nzuri hakukuwa na majeruhi au vifo vilivyopatikana.

lilihusika katika ajali Jumatano asubuhi.
Basi la Chuo Kikuu cha Moi lilihusika katika ajali Jumatano asubuhi.
Image: HISANI

Chuo kikuu cha Moi kimevunja ukimya baada ya basi lao moja kuhusika katika ajali ya barabarani katika eneo la Kimende, kaunti ya Kiambu.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatano mchana, taasisi hiyo ambayo ina makao yake mjini Eldoret ilithibitisha kuwa ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa nne alfajiri.

Makamu chansela, Profesa Isaac S. Kosgey alifichua kuwa basi hilo lilikuwa na wanafunzi 65 kutoka Shule ya Sanaa na Sayansi ya Jamii waliokuwa wakienda kwa Safari ya Kimasomo..

“Leo asubuhi mwendo wa saa tatu na hamsini asubuhi, basi letu la Chuo Kikuu KCK 583U likiwa na wanafunzi 65, lilihusika katika ajali mbaya ya barabarani katika eneo la Kimende kwenye Barabara kuu ya Nakuru - Nairobi tukiwa katika Safari ya Kielimu na wanafunzi kutoka Shule ya Sanaa na Jamii. Sayansi, Idara ya Kiswahili,” Bw Kosgey alisema.

Alitangaza kuwa kwa bahati nzuri hakukuwa na majeruhi au vifo vilivyopatikana.

“Nimefarijika kuwajulisha kuwa hakuna majeruhi wala vifo, na wanafunzi wote wako salama. Basi limetumwa kuwarudisha kwenye Kampasi Kuu. Ningependa kutoa shukrani zangu kwa kujali kwenu na usaidizi wenu wakati huu," alisema.

Kufuatia tukio hilo, taasisi hiyoya elimu ya juu sasa imepiga marufuku safari zote za masomo wakati wa Sikukuu ya Pasaka kama tahadhari.

“Kutokana na tukio hili, nawaomba Madereva na watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu zaidi wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kama hatua ya tahadhari, Safari zote za Kielimu zimesitishwa hadi baada ya Likizo ya Pasaka," makamu wa chansela alisema.

Wanafunzi kumi na wawili hata hivyo waliripotiwa kupata majeraha madogo katika ajali hiyo.

Naibu kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Lari, Francis Njomo alisema wanafunzi hao walikimbizwa katika hospitali ya Orthodox katika mji wa Kimende.

Njomo alithibitisha kuwa basi hilo lilikuwa na wanafunzi 50.

Aliongeza kuwa dereva wa basi hilo alishindwa kulidhibiti katika mazingira yasiyoeleweka na basi likatua kwenye mtaro.

Njomo alisema polisi wa trafiki wameanzisha uchunguzi kubaini kilichotokea kabla ya ajali hiyo.

"Tunachunguza ili kubaini jinsi dereva alivyopoteza udhibiti na basi hilo kushuka barabarani," alisema.