Murang'a: Jamaa aliyekuwa jela miaka 7 kwa mauaji aua wengine 2 baada ya kuachiliwa

Wakaazi wlaisema mwanamume huyo alimaliza kifungo cha miaka 7 jela miaka 2 iliyopita baada ya kupatikana na hatia ya kuua wakongwe wawili.

Muhtasari

• Baada ya kumaliza kifungo na kurudi nyumbani, mwanamume huyo aliwaua kwa kuwacharanga mapanga wanaume wengine wawili kabla ya kuingia mitini.

Panga. Silaha ya muuajiiliyotumika
Panga. Silaha ya muuajiiliyotumika
Image: MAKTABA

Wakaazi eneo la Mathioya kaunti ya Murang’a wamebaki na wasiwasi baada ya mwanamume ambaye alikuwa jela kwa miaka 7 kwa hatia ya mauaji kuua watu wengine wawili tena, miaka miwili baada ya kumaliza kifungo chake na kurudi nyumbani.

Kwa mujibu wa ripoti iliyopeperushwa kwenye runinga ya KBC, mwanamume huyo awali alikuwa amefungwa jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwaua wakongwe wawili.

Baada ya kumaliza kifungo na kurudi nyumbani, mwanamume huyo aliwaua kwa kuwacharanga mapanga wanaume wengine wawili kabla ya kuingia mitini.

Ripoti zinaonyesha kuwa alitenda mzaha na kuwakatakata Stanley Kamau Irungu na Benard Mahiu Mwangi (wote umri wa miaka 44) hadi kufa baada ya kutofautiana wakiwa katika baa ya eneo hilo.

Babake Kamau, Irungu Maina, alishindwa kuzuia machozi alipokuwa akisimulia jinsi kichwa cha mwanawe kilivyokuwa na michubuko mirefu, huku mwili wa marehemu ukiachwa ukiwa umelala njiani.

“Nina huzuni sana kwa sababu huyu ndugu yangu mdogo ndiyo tulikuwa tunasaidiana na yeye kwa mambo mengi, naomba serikali ijaribu imshike arudi jela,” alisema ndugu wa mmoja wa wanaume waliocharangwa mapanga.

Wakaazi hao waliokuwa na wasiwasi wa kutojua ni nani atakuwa mwathiriwa wa mshukuwa baadae, walitoa wito kwa serikali kupitia maafisa wake wa polisi kufanya msako na kumuondoa jamaa huyo miongoni mwa jamii wakimtaja kama tishio kwa maisha yao.