Nairobi: Mwanaume anayeuza smokie ashabikiwa kwa kumsaidia mjamzito kujifungua barabarani

“Kurudi nikapata mama alikuwa hapo anainuka akisema mtoto ametoka na miguu, nikamwambia hebu nione, kuona kweli mtoto alikuwa ametoka na miguu kichwa kimebaki ndani, daktari hayuko na tuko kina mama wawili na mimi..."

Muhtasari

• Gekonge alisimulia kwamba kina mama waliokuwa katika sehemu ya tukio walimtuma akimbie amuite daktari lakini kufika daktari akamwambia kwamba alikuwa bize.

Kijana amsaidia mama mjamzito kujifungua
Kijana amsaidia mama mjamzito kujifungua
Image: screengrab//NTVKenya

Mwanamume mmoja mwenye umri wa miaka 27 ambaye anafanya kazi ya kuchuuza vyakula aina ya smokie na samosa jijini Nairobi amesherehekewa kama shujaa kwa kitendo chake cha kumsaidia mwanamke mjamzito kujifungua salama barabarani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya kutia moyo iliyopeperushwa kwenye runinga ya NTV Kenya, kijana huyo kwa jina Dominic Gekonge alimsaidia mwanamke huyo mjamzito aliyepatwa na maumivu ya kujifungua ghafla barabarani.

Gekonge alisimulia kwamba kina mama waliokuwa katika sehemu ya tukio walimtuma akimbie amuite daktari lakini kufika daktari akamwambia kwamba alikuwa bize.

Aliporudu, kina mama wale walikuwa wanamsubiri na kumuuliza kama amempata daktari na hapo ndipo aliona mama mjamzito amezidiwa ikambidi kulivalia njuga suala la kumsaidia kujifungua, licha ya kutokuwa na ujuzi wowote.

“Nilirudi nikapata wanangoja daktari, kuangalia hapo chini mtoto alikuwa ameshatoa miguu, hakuna njia nyingine ambayo tulikuwa nayo, sasa ikabidi nirudi pale hospitalini nichukue wembe, daktari pia akanipa clips Fulani zilikuwa hapo,” alieleza.

“Kurudi nikapata mama alikuwa hapo anainuka akisema mtoto ametoka na miguu, nikamwambia hebu nione, kuona kweli mtoto alikuwa ametoka na miguu kichwa kimebaki ndani, daktari hayuko na tuko kina mama wawili na mimi. Nikamshika pua na mdomo vile niliona madaktari walikuwa wanafanya kwa mke wangu akijifungua, na hivyo ndio mtoto alitoka,” Dominic alisimulia Zaidi.

Baada ya kumsaidia kujifungua salama, waliita gari na kumpeleka mama na mtoto hospitalini wakiwa salama salimini.

Kijana huyo muuza smokie baada ya kukamilisha shughuli yote, aligeuka shujaa na kusherehekewa na kina mama waliokuwa wamezingira eneo hilo.