Chuo Kikuu cha Kenyatta chavunja kimya baada ya moto mkubwa kuonekana katika taasisi hiyo

Taasisi hiyo imethibitisha kuwa kweli kisa cha moto kilitokea kwenye ghorofa ya juu ya Maktaba ya Old Moi.

Muhtasari

•Taasisi hiyo ilifichua kuwa hakukuwa na mfanyikazi wala mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo la moto

•Hata hivyo, mali ya thamani ambayo haijafichuliwa iliharibiwa wakati wa tukio hilo la Ijumaa usiku.

Lango la Chuo Kikuu cha Kenyatta
Image: MAKTABA

Chuo Kikuu cha Kenyatta, mnamo Jumamosi jioni, kilitoa taarifa kuzungumzia tukio la moto ambalo liliripotiwa katika taasisi hiyo usiku wa Ijumaa.

Siku ya Ijumaa usiku, habari zilizuka kwenye mitandao ya kijamii na majukwaa mengine ya habari kwamba moto mkubwa ulionekana kwenye jengo moja la taasisi hiyo.

Taasisi hiyo imethibitisha kuwa kweli kisa cha moto kilitokea kwenye ghorofa ya juu ya Maktaba ya Old Moi mwendo wa saa tano usiku wa kuamkia Jumamosi.

“Kufuatia juhudi za haraka na zilizoratibiwa za wazima moto wa KU pamoja na usaidizi na ushirikiano mkubwa kutoka Kaunti ya Kiambu na Kikosi cha Zimamoto cha Kahawa Millitary Barracks, moto huo ulizuiliwa haraka.

Mwitikio wa ushirikiano wa vyombo hivi mbalimbali ulipunguza kwa kiasi kikubwa ukali wa hali hiyo,” Chuo Kikuu cha Kenyatta kilisema katika taarifa iliyotiwa saini na Naibu Chansela Prof. Waceke Wanjohi.

Taasisi hiyo ilifichua kuwa hakukuwa na mfanyikazi wala mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo la moto kwani lilitokea baada ya saa za kazi ambapo kila mtu alikuwa ametoka katika jengo hilo lililokuwa na ofisi za idara mbalimbali na utawala.

Hata hivyo, mali ya thamani ambayo haijafichuliwa iliharibiwa wakati wa tukio hilo la Ijumaa usiku.

“Leo asubuhi (Jumamosi), wasimamizi wa chuo walikuwa eneo la tukio na kutathmini hali ilivyokuwa. Timu yetu ya usalama sasa imelilinda eneo hilo kikamilifu na uchunguzi umeanza. Tunataka kusisitiza kwamba usalama na ustawi wa wanafunzi wetu na wafanyikazi unasalia kuwa kipaumbele chetu kikuu, "ilisema taarifa hiyo.

Chuo hicho pia kimewashukuru wale wote walioshiriki katika wito wa haraka na kuudhibiti moto huo ambao chanzo chake bado hakijafahamika.

"Chuo kikuu kitatoa taarifa zaidi kadri zitakavyopatikana," walisema.