Idara ya utabiri wa hali ya anga yatangaza maeneo yatakayokumbwa na mvua wiki hii

Takriban vifo 228 vimeripotiwa, watu 164 wamejeruhiwa na 72 bado hawajulikani walipo huku mvua ikiendelea katika maeneo mbalimbali

Muhtasari

•Walisema kuwa matukio ya mvua kubwa ya pekee yanaweza kutokea katika eneo la Ziwa Victoria, Magharibi mwa Kenya, Kati, na Sehemu za eneo la Pwani.

•Mvua inayoendelea kunyesha katika eneo la Kati na kufurika kwa Mabwawa ya Seven Forks huenda ikasababisha mafuriko katika eneo la Tana Delta,

Image: HISANI

Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga ya Kenya imetoa taarifa kuhusu utabiri wa hali ya anga wa wiki mpya kati ya Mei 5 na Mei 12 huku nchi ikiendelea kukumbwa na viwango tofauti vya mvua.

Katika taarifa yake ya Jumapili, Mei 5, idara hiyo ilitangaza kuwa mvua zinatarajiwa kunyesha mara kwa mara katika maeneo ya Magharibi, Bonde la Ufa, Kati, Pwani, sehemu za Nyanda za Juu Kusini-Mashariki, sehemu za Kaskazini Mashariki na Maeneo ya Ziwa Victoria.

Walisema kuwa matukio ya mvua kubwa ya pekee yanaweza kutokea katika eneo la Ziwa Victoria, Magharibi mwa Kenya, Kati, na Sehemu za eneo la Pwani.

Sehemu nyingi za Kaskazini Mashariki, Kaskazini-Magharibi na sehemu za mikoa ya Kusini Mashariki zimetabiriwa kuwa kavu kwa ujumla, huku mvua ikinyesha mara kwa mara hadi wastani.

Idara ya utabiri wa hali ya anga ilionya kuwa mvua inayoendelea kunyesha katika eneo la Kati na kufurika kwa Mabwawa ya Seven Forks huenda ikasababisha mafuriko katika eneo la Tana Delta, na kuathiri kaunti za Garissa, Tana River na Lamu.

Mvua nyepesi hadi nzito imeshuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini katika muda wa wiki kadhaa zilizopita. Mvua hizo kubwa zimesababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika baadhi ya maeneo, na kusababisha kupoteza kwa maisha na mali.

Kufikia sasa,takriban vifo 228 vimeripotiwa, watu 164 wamejeruhiwa na 72 bado hawajulikani walipo huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika taarifa ya siku ya Jumapili, Wizara ya Masuala ya Ndani inayoongozwa na waziri Kindiki Kithure imesema jumla ya boma 42,526 zimehamishwa na takriban watu 227,238 wameathiriwa na mvua kubwa inayoendelea.