Serikali yaomba kila mtu mzima kupanda miti 50 na kila mtoto kupanda miti 10 Ijumaa

Ikumbukwe rais Ruto alishaweka nadhiri kwamba ifikapo mwaka 2015, angependa kuona taifa la Kenya likiwa limepandwa miti zaidi ya bilioni 15.

Muhtasari

• "Hili litakuwa zoezi endelevu ambapo Mawaziri watatenga siku katika mwezi mmoja kushiriki katika ukuzaji wa miti," Tuya alisema katika taarifa yake.

Image: PCS

Serikali kupitia kwa waziri wa mazingira Soipan Tuya imeomba kila Mkenya mtu mzima kujishughulisha katika upanzi wa miti angalau 50 huku kila mtoto akiomba kupanda angalau miti 10 mnamo Ijumaa ya Mei 10.

Awali, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alitangaza kwamba Ijumaa itatengwa rasmi kama sikukuu kwa ajili ya kutoa fursa kwa upanzi wa miti lakini pia kuwakumbuka waathiriwa wa mafuriko kutokana na mvua nyingi zinazozidi kunyesha nchini.

Itakuwa Siku ya Kitaifa ya Kukuza Miti ya pili nchini Kenya, kufuatia uzinduzi wa ‘Likizo ya Kijani’ mnamo Novemba 13, 2023.

"Ili kufuatilia idadi ya miti, wananchi wanahimizwa kuhakikisha kuwa miti yote iliyopandwa siku hiyo inarekodiwa na picha zinawekwa kwenye programu ya Jaza Miti,"

Ili kuonyesha jukumu la mstari wa mbele la serikali katika Mpango wa Kitaifa wa Kupanda Miti Bilioni 15, kila Katibu wa Baraza la Mawaziri amepewa maeneo maalum kulingana na maagizo ya Baraza la Mawaziri.

Kwa mantiki hiyo, Makatibu wa Baraza la Mawaziri wamepewa jukumu la kuratibu Wizara zao, zikiwemo Wakala wa Serikali wa Semi-Autonomous Government (SAGAs) zilizo chini yao pamoja na jumuiya mwenyeji ili kuhakikisha kuwa maeneo haya yanarejeshwa kikamilifu.

"Hili litakuwa zoezi endelevu ambapo Mawaziri watatenga siku katika mwezi mmoja kushiriki katika ukuzaji wa miti," Tuya alisema katika taarifa yake.