Mkate kuuzwa Sh80, ikiwa ushuru wa 25% kwa mafuta ya kupikia utapitishwa

Watengenezaji wameonya kuongezeka kwa bei ya mkate ,ikiwa ushuru wa 25% kwa mafuta utapitishwa bungeni.

Muhtasari

•Asilimia 25 ya ushuru wa bei ya bidhaa utaamuliwa kwenye mswada wa fedha, 2024

•Watengenezaji wanataka ushuru wa asilimia 25 wa mafuta ya mboga kufutiliwa mbali

Watengenezaji wa mafuta ya kula nchini wameonya kuwa, pendekezo la asilimia 25 ya ushuru wa bidhaa kwa mafuta ya mboga, chini ya mswada wa fedha wa 2024,utaonge bei ya mafuta ya kupikia hadi asilimia 80.

Taarifa ambayo walitoa Jumapili,inaashiria kuwa ushuru unaolenga mafuta ya kupikia, utafanya bei ya bidhaa kuongezeka hivo kutoweza kufikiwa na mamilioni ya Wakenya.

Aidha,walionya kuwa itakuwa na athari mbaya kwa gharama ya vyakula vya kawaida kama mkate.Ikiwa mswada huo utapitishwa,bei ya mkate wa gramu 400 itapanda kutoka Ksh.70 hadi Ksh.80

'Ushuru wa bidhaa unaopendekezwa pia utasababisha ongezeko la ghafla la bei kwa bidhaa nyingine muhimu za nyumbani ambazo malighafi yake ni mafuta ya mboga  kama vile sabuni ,ikiongezeka kutoka Ksh.180 hadi Ksh.270...' watengenezaji hao walisema.

Watengenezaji wanataka ushuru wa asilimia 25 wa mafuta ya mboga kufutiliwa mbali, wakisema kuwa utakandamiza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.

Waliutaja kuwa kinyume na sera ya serikali ya kukuza uongezaji wa thamani wa ndani kwa biashara ya kilimo nchini.