Polisi wamsaka mwanamke anayedaiwa kumtelekeza mtoto, 3, katika hospitali ya Nyamira

Hata hivyo, mtoto huyo hakuwa na stakabadhi zozote ambazo zingesaidia maafisa wa polisi au hata uongozi wa hospitali kumtambua kwa urahisi.

Muhtasari
  • Kulingana na Naibu Msimamizi wa Hospitali Angela Kerubo, mtoto huyo alitelekezwa katika kitengo cha wagonjwa wa nje na hivyo hivyo kuripotiwa katika afisi za Watoto zilizoko Nyamira

Polisi katika kaunti ndogo ya Nyamira Kusini wanamsaka mwanamke wa umri wa makamo anayedaiwa kumtelekeza mtoto wa miaka mitatu katika hospitali ya rufaa ya Nyamira.

Kulingana na Naibu Msimamizi wa Hospitali Angela Kerubo, mtoto huyo alitelekezwa katika kitengo cha wagonjwa wa nje na hivyo hivyo kuripotiwa katika afisi za Watoto zilizoko Nyamira na ripoti zilizofuata kufanywa katika kituo cha polisi cha Nyamira.

Hata hivyo, mtoto huyo hakuwa na stakabadhi zozote ambazo zingesaidia maafisa wa polisi au hata uongozi wa hospitali kumtambua kwa urahisi.

Mkuu wa polisi wa kaunti ndogo ya Nyamira Kusini Isaac Sang alisema mtoto huyo amekabidhiwa hospitalini kwa huduma ya usalama ya usiku mmoja kabla ya kupelekwa Hope Alive kaunti ya Kisumu.

“Tutampeleka mtoto huyo katika Kituo cha Kisumu Hope Alive huku maafisa wetu wakiendelea na uchunguzi kujua ni nani aliyemwacha mtoto katika kituo hicho. Tutakupa ripoti kuhusu maendeleo ya suala hilo kwa wakati,” bosi wa polisi alisema.

Alisema jitihada za kumtafuta mama wa mtoto huyo zinaendelea, aliwataka wakazi kuwajibika kwa watoto wao badala ya kuwatelekeza.