Balozi wa Uingereza akutana na jamaa wa Wanjiru anayedaiwa kuuawa na mwanajeshi wa Uingereza

Taarifa fupi kutoka kwa Ubalozi wa Uingereza ilisema: "Mkutano huo ulitoa fursa ya kusikiliza familia na kutoa rambirambi".

Muhtasari
  • Neil Wigan alikutana  mjini Nairobi na jamaa wa Agnes Wanjiru siku ya Jumatano , ambaye mwili wake ulipatikana mwaka wa 2012 karibu na kambi ya Uingereza kaskazini mwa Kenya.
AGNES WANJIRU
Image: MAKTABA

Balozi wa Uingereza nchini Kenya amekutana na familia ya Agnes Wanjiru anayedaiwa kuuawa na mwanajeshi wa Uingereza zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Neil Wigan alikutana  mjini Nairobi na jamaa wa Agnes Wanjiru siku ya Jumatano , ambaye mwili wake ulipatikana mwaka wa 2012 karibu na kambi ya Uingereza kaskazini mwa Kenya.

Taarifa fupi kutoka kwa Ubalozi wa Uingereza ilisema: "Mkutano huo ulitoa fursa ya kusikiliza familia na kutoa rambirambi".

Ni mara ya kwanza kwa mtu yeyote kutoka serikali ya Uingereza kukutana na familia ya Bi Wanjiru, ambaye jamaa zake kwa miaka kadhaa wamekuwa wakishinikiza kuwe na mkutano rasmi.

Mkutano huo unafuatia pendekezo la mapema mwaka huu la Waziri wa zamani wa Jeshi la Uingereza James Heappey kukutana binafsi na familia hiyo.

“Tuna furaha kwa mkutano; imechukua miaka 12! Tumeona serikali ya Uingereza ina nia njema na tunatumai kuwa kesi hiyo itafuatiliwa haraka ili haki itendeke” alisema.

Wakili wa familia Mbiu Kamau alisema anamshukuru Kamishna Mkuu kwa kutoa rambirambi na masikitiko “kweli alikuwa na kikao cha mazungumzo ya wazi na familia na walifurahishwa na ukarimu wake na uwazi aliowasikiliza, walizungumza naye kwa uhuru na alijisikia raha” alisema.

Miaka saba baada ya mauaji ya Bi Wanjiru uchunguzi wa Kenya ulihitimisha kwamba aliuawa na askari mmoja au wawili wa Uingereza.

Akiwa katika ziara rasmi nchini Kenya mwezi Februari mwaka huu Waziri wa zamani wa Jeshi la Uingereza alisisitiza kuwa mkutano huo hautahusu kukubali hatia kwa niaba ya serikali ya Uingereza huku uchunguzi wa kisheria ukiendelea.

Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya ilifungua uchunguzi, lakini haijamshtaki mshukiwa yeyote na Kenya haijaomba kurejeshwa kwa washukiwa hao.

Kamishna Mkuu amesisitiza kuendelea kujitolea kwa Uingereza kushirikiana na uchunguzi wa Kenya kuhusu kifo cha Agnes Wanjiru.

Wakili wa familia Mbiu Kamau alisema anatumai mkutano huu wa kwanza na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Uingereza unaashiria mwanzo mpya katika harakati za kutafuta haki kwa familia.

“Familia imekuwa ikihisi kutelekezwa na kupuuzwa na serikali za Uingereza na Kenya kwa sababu ya hadhi yao ya kijamii.

Tunatumai masuala mengine yanaweza kushughulikiwa baada ya hapo”. Alisema.