Sitatishwa - Mbunge Sudi asema baada ya Gachagua kuwakosoa viongozi wa Rift Valley

Gachagua hakutaja jina lolote na kuwataka wabunge kushikamana na maeneo bunge yao na kuacha utalii wa kisiasa.

Muhtasari
  • Sudi, hata hivyo, alishikilia kuwa wanaunga mkono kwa dhati Rais William Ruto na Gachagua akisema wawili hao ni wagombeaji wa Kenya Kwanza 2027.
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi
Image: MAKTABA

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ameshikilia kuwa hataacha kuzunguka nchi nzima kusaidia makundi yaliyo hatarini na makanisa katika masuala ya maendeleo.

Haya yanajiri siku moja baada ya DP Rigathi Gachagua kukosoa baadhi ya viongozi kutoka Rift Valley ambao alitilia shaka chanzo chao cha pesa akisema wamekuwa wakiruka kutoka eneo moja hadi jingine kwa kutumia helikopta kula pesa.

Gachagua hakutaja jina lolote na kuwataka wabunge kushikamana na maeneo bunge yao na kuacha utalii wa kisiasa.

"Rasilimali hizi zinatoka wapi, za kufanya siasa, wakati Wakenya wanateseka? Chopper wanaajiriwa kushoto, kulia na katikati. Mamilioni ya pesa yanaliwa na Wakenya wanateseka," Gachagua alisema.

“Nawaomba wabunge wabaki kwenye Jimbo lao na kuwatumikia wananchi wao. Tabia ya utalii wa kisiasa lazima ikome. Hiki ndicho kinatupa shida.”

Katika kujibu matamshi hayo, Sudi alijibu hoja akisema hatatishika kuacha kuzunguka nchi nzima kuunga mkono makanisa.

Sudi alisema alijifunza sanaa ya kuunga mkono makanisa kutoka kwa Rais William Ruto na kuongeza kuwa serikali ya Kenya Kwanza haingepata mamlaka ikiwa wangesalia katika maeneobunge yao.

"Jana niliona wajumbe wengine wamesanyana huko Kesses hapa wanasema kuna mtu anakoroga, sijui kuna mtu pale. Sasa ukienda useme huyu Oscar Sudi asizunguke, akae kwa constituency na wakati unaongea uko kwa constituency ya mwingine na mko wabunge karibu 30 hiyo sini contradiction."

Aliendelea:

"Wale wote walikua Kesses pale walikua wanatumia helikopta tukiwa upinzani na walizunguka Kenya mzima ndo wakajulikana mpaka wakapata cheo chako nayo. Kama hutaki kuzunguka kaa nyumbani kwako. Tafuteni mtu mwingine wa Kutisha, mimi nilipita vitisho kitambo.

Sudi alikuwa akizungumza wakati wa harambee ya kusaidia kukamilika kwa ujenzi wa Kanisa la AIC Kipkorgot, wadi ya Kapsoya, eneo bunge la Ainakboi.

Mbunge huyo aliendelea kutetea chanzo cha fedha zake akibainisha kuwa hakuwahi madarakani alipojiunga na siasa.

"Nawauliza nyinyi mko hapa, niliomba kura 2012 ya kwanza mlisikia sikukuwa pesa? Mulisikia niliomba mtu mafuta? Naona mtu anataka kunisomea hapa akisema huyu mtu anatoa pesa, mara anatembea na ndege. Kwani hii ndege ilitengenezwa nani atembee nayo?

Sudi, hata hivyo, alishikilia kuwa wanaunga mkono kwa dhati Rais William Ruto na Gachagua akisema wawili hao ni wagombeaji wa Kenya Kwanza 2027.

Hata hivyo, alisema 2032 ni jambo lililo mikononi mwa Mungu na kuongeza kuwa litajulikana muda utakapofika.