'Tuheshimiane!' Rais Ruto awaonya wanyakuzi wa ardhi

Ripoti zilionyesha kuwa mmiliki wa jengo hilo, Patrick Wangamati, alidaiwa kujinyakulia shamba hilo kinyume cha sheria lakini alikanusha vikali madai hayo.

Muhtasari
  • Onyo la Ruto linakuja takriban mwezi mmoja baada ya jengo la Ksh.500 milioni la familia ya aliyekuwa Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati kubomolewa ili kupisha ukarabati wa uwanja wa Masinde Muliro.
RAIS WILLIAM RUTO
Image: PCS

Rais William Ruto Jumamosi alitoa onyo kali kwa wanyakuzi wa ardhi, akiangazia athari zao mbaya katika malengo ya maendeleo ya Kenya.

Akihutubia Wakenya waliokuwa wamekusanyika katika uwanja wa Masinde Muliro kaunti ya Bungoma kuadhimisha sherehe za 61 za Madaraka, Ruto aliwataka watu wanaohusika na unyakuzi wa ardhi katika eneo hilo kuondoka mara moja na kukabidhi vifurushi hivyo kwa serikali.

"Wananchi wanaozunguka uwanja huu, hasa wale ambao wameamua kujipatia baadhi ya ardhi ya umma. Tafadhali, tuheshimiane kidogo, kila mtu ambaye akona shamba la serikali, funga virago vyako polepole," alisema.

"Hatutaki vita na mtu kwa sababu mali ya umma ni ya wananchi wa Kenya."

Onyo la Ruto linakuja takriban mwezi mmoja baada ya jengo la Ksh.500 milioni la familia ya aliyekuwa Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati kubomolewa ili kupisha ukarabati wa uwanja wa Masinde Muliro.

Ripoti zilionyesha kuwa mmiliki wa jengo hilo, Patrick Wangamati, alidaiwa kujinyakulia shamba hilo kinyume cha sheria lakini alikanusha vikali madai hayo.

“Sikupata ardhi hii kinyume cha sheria. Ilitangazwa. Nilituma maombi na kupata, nilikuwa nikikimbilia kituo cha mafuta kiitwacho Ajip petrol station,” alisema kisha.

"Kama mimi ni mnyakuzi ningeweza kumiliki vipande vikubwa vya ardhi huko Webuye kwa sababu huo ndio mji ambao nimeendesha shughuli zake kwa muda mrefu. ”

Aidha alikashifu serikali ya kaunti ya Bungoma kwa madai ya kupuuza agizo la mahakama lililositisha ubomoaji huo.